Home Mchanganyiko Naibu Waziri Aweso azitaka Mamlaka za maji nchini kuunganisha maji ndani ya...

Naibu Waziri Aweso azitaka Mamlaka za maji nchini kuunganisha maji ndani ya siku saba

0

Naibu Waziri wa Maji Mh. Jumaa Aweso akimtua ndoo ya maji mmoja wa akina mama katika moja ya sehemu za kuchotea maji katika kijiji cha Kalumbaleza, Wilayani Sumbawanga. 

****************************************

Naibu Waziri wa Maji Mh. Jumaa Aweso amewaagiza Wakurugenzi wa Mamlaka za maji nchini kuhakikisha wananchi ambao wamekamilisha taratibu za kulipia uunganishaji wa maji wanapatiwa huduma hiyo ndani ya siku saba, kwani hiyo ni haki ya mwananchi na ni wajibu wa serikali kuhakikisha mwananchi anapata maji hayo.

“Si jambo la busara hata kidogo mwananchi amefuata taratibu za kulipia uuunganishwaji wa maji anatumia miezi mitatu, miezi minne, dana dana zimekuwa lukuki haiwezekani, tunataka ndani ya siku saba, na ieleweke mtu ameshindwa atupishe, tuweke watu ambao wanaweza wakaifanya hiyo kazi, kwahiyo nawaomba wananchi wa Tanzania muelewe na mfahamu kwamba utakapokuwa umekamilisha taratibu za kulipia maunganisho wa maji basi ndani ya siku saba Mamlaka iweze kuhakikisha kwamba mwananchi huyu anapata huduma ya maji,” Alimalizia.

Ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji mkoani Rukwa kabla ya kuanza ziara yake ya siku mbili katika mkoa ili kukagua na kutembelea miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa ndani ya Mkoa.

Wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji Mkoani Rukwa Kaimu Meneja wa Wakala wa maji vijiji Mhandisi Boaz Matundali alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 Mkoa wa Rukwa umepanga kutekeleza jumla ya miradi 30 ambapo kati ya hiyo miradi 14 ni mipya na 16 ni ya ukarabati na upanuzi na kuongeza kuwa kiasi kilichotengwa kwaajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ni Shililingi 10, 102,639,591/=.

Wakati serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani mwaka 2015 upatikanaji wa maji safi na salama Mkoani Rukwa ulikuwa asilimia 40.4 na kufikia mwezi Juni, 2020, asilimia 63 ya wakazi vijijini pamoja na asilimia 80 ya wakazi wa mjini wanapata maji safi na salama huku serikali ikiwa imewekeza kiasi cha Shilingi Bilioni 46.5.