Home Mchanganyiko MLOGANZILA YAPATIWA MSAADA VIFAA TIBA

MLOGANZILA YAPATIWA MSAADA VIFAA TIBA

0

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza kabla ya kukabidhiwa msaada wa vifaa tiba kutoka Taasisi ya Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH), kulia ni Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi, kushoto ni Mwakilishi wa KOFIH Bi. Kim Jungyoon.

Prof. Museru na Dkt. Magandi wakiwa wameshika moja kati ya vifaa tiba vilivyokabidhiwa hospitalini hapa kinachotumika kupima kiwango stahiki cha gesi katika vifaa tiba vinavyotumia gesi (Portable Gas Flow Analyzer).

…………………………………………………………………………

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya TZS. Mil 331,383,000 kutoka Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH) ambao unalenga kuisaidia hospitali kuendelea kutoa huduma bora na za ubingwa wa juu kwa wagonjwa wanaofika kupatiwa matibabu hospitalini hapa.

Msaada huo umejumuisha vifaa tiba vya kufanyia upasuaji masikio, pua na koo vilivyogharimu Dola za Marekani 41,826 sawa na TZS. Mil. 96,199,800 na vifaa vya ufundi kwa ajili ya matengenezo ya vifaa tiba vyenye thamani ya dola za marekani 102,254 sawa na TZS. Mil. 235,184,200.

Akipokea msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru ameishukuru taasisi hiyo kwa kuendeleza mahusiano na MNH pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano kwa kuwajengea uwezo wataalamu kupitia mafunzo mbalimbali na pia katika kuimarisha utoaji huduma kwa kutumia vifaa tiba vilivyopo hospitalini hapa. 

“Changamoto tuliyonayo ni utengenezaji wa vifaa tiba tulivyonavyo pindi vinapopata hitilafu lakini kupitia ushirikiano mzuri tulionao na KOFIH umewezesha wataalamu wetu kupata ujuzi na vifaa kwa ajili ya matengenezo ambayo yamewezesha hospitali kuendelea kutoa huduma pasipo shida yoyote,” amesema Prof. Museru.

Mwakilishi wa Taasisi ya Korea Foundation for International Healthcare, Bi. Kim Jungyoon amesema wanayofuraha kukabidhi msaada huu ambao utasaidia wataalamu wa upasuaji masikio,pua na koo pamoja na wataalamu vifaa tiba kufanya kazi zao kwa ufanisi.

“Tunaishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuendeleza mahusiano haya nasi tunaahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha wataalamu wanapatiwa mafunzo na vifaa tiba vitakavyowasaidia wakati wa kutimiza majukumu yao ya kila siku,” amesema Bi. Jungyoon.

Mwishoni mwa mwaka jana KOFIH ilitoa mafunzo ya mwezi mmoja kwa  wataalamu wa vifaa tiba kutoka Dar es Salaam, Dodoma, Tabora, Lindi, Tanga, Geita, Mwanza, Arusha, Pwani, Mtwara, Singida, Mbeya, Kilimanjaro, Shinyanga na Katavi.