……………………………………………………………………………..
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuwatia mbaraoni watuhumiwa wanne kwa tuhuma ya kupatikana na mali mbalimbali za wizi. Watuhumiwa waliokamatwa katika msako huo ni:-
- FRIDAY FREDY @ MWANGISI [36] Mfanyabiashara na Mkazi wa Maanga
- RAMADHAN RAMAN [34] Fundi simu na Mkazi wa Mafiati.
- GODFREY JOHN [36] Mkazi wa Mwanjelwa.
- HAMIS MEJA [30] Mkazi wa Airport ya Zamani.
Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 02.08.2020 majira ya saa 11:00 Asubuhi huko maeneo ya Mtaa wa Maendeleo, Kata ya Maanga, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya katika nyumba ya kulala wageni iitwayo “AFTER WORK” inayomilikiwa na mtuhumiwa FRIDAY FREDY @ MWANGISI.
Katika upekuzi uliofanyika katika nyumba hiyo ya kulala wageni watuhumiwa walikutwa na vitu vifuatavyo:-
- FRIDAY FREDY @ MWANGISI [36] Mfanyabiashara na Mkazi wa Maanga alikutwa na vifaa mbalimbali vya kufungashia dawa za kulevya aina ya Heroine/Cocaine, Simu nane [08] za aina mbalimbali zikiwa hazina laini, Laini za simu kumi na tano [15] za mitandao tofauti.
- RAMADHAN RAMAN [34] Fundi simu na Mkazi wa Mafiati baada ya kukamatwa akiwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni alikwenda na askari hadi nyumbani kwake na katika upekuzi alikutwa na Mashine moja ya Kidaktari ya kupimia mapigo ya moyo [Stethoscope], Laptop mbili [02] aina ya Lenovo na Dell, Simu tatu [03], mbili aina ya Samsung na iPhone moja zikiwa hazina laini.
Aidha watuhumiwa GODFREY JOHN [36] Mkazi wa Mwanjelwa na HAMIS MEJA [30] Mkazi wa Airport ya Zamani walikutwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni wakiwa wanajidunga dawa za kulevya kwa kutumia sindano. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Sambamba na hilo, katika msako uliofanyika maeneo ya Mtaa wa Maendeleo Jijini Mbeya Polisi tulifanikiwa kumkamata OBEID WATSON @ NTAENA [34] Mkazi wa Mbalizi akiwa na Madini yanayodhaniwa kuwa bandia yenye uzito wa gramu 27.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 02.08.2020 majira ya saa 13:00 Mchana katika “Bar” iitwayo “AFTER WORK” inayomilikiwa na FRIDAY FREDY @ MWANGISI [36] Mfanyabiashara na Mkazi wa Maanga baada ya askari kumtilia mashaka wakati anaingia katika “Bar” hiyo na katika upekuzi alikutwa na madini yanayodhaniwa kuwa ni bandia akiwa ameyahifadhi katika mfuko wa “Nylon” wenye maandishi yanayosomeka “Grade “A” Yenye Thamani ya Tshs.20,000,000/= (MILIONI ISHIRINI) BENKI YOYOTE DUNIANI”
Mtuhumiwa amekiri kutumia madini hayo kutapeli watu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
WITO WA KAMANDA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anaendelea kutoa msisitizo kwa wamiliki wa vilabu vya pombe na Bar kuwa makini na wateja wao na waonapo matapeli, wezi, wagomvi watoe taarifa kwa viongozi wa Mitaa, Jeshi la Polisi ili kunusuru/kuleta usalama na amani kwa watu wengine.