Home Mchanganyiko Klabu ya Mazoezi ya Xtreme Workout Bootcamp watembelea wodi ya watoto JKCI

Klabu ya Mazoezi ya Xtreme Workout Bootcamp watembelea wodi ya watoto JKCI

0

Wanachama wa klabu ya mazoezi ya Xtreme workout bootcamp wakifanya usafi katika jengo la watoto wenye magonjwa ya moyo walipotembelea watoto waliolazwa katika jengo hilo kwa ajili ya kutoa zawadi kwa watoto pamoja na kuchangia gharama za kutengeneza kadi mbili za bima ya afya kwa watoto leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam Wanachama wa klabu ya mazoezi ya Xtreme workout bootcamp wakifanya usafi katika jengo la watoto wenye magonjwa ya moyo walipotembelea watoto waliolazwa katika jengo hilo kwa ajili ya kutoa zawadi kwa watoto pamoja na kuchangia gharama za kutengeneza kadi mbili za bima ya afya kwa watoto leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam Mama mwenye mtoto aliyelaza katika wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo Halima Selemani akipokea zawadi za mwanae kutoka kwa wanachama wa klabu ya mazoezi ya Xtreme workout bootcamp waliotembelea JKCI kwa ajili ya kufanya usafi katika jengo la watoto pamoja na kutoa zawadi kwa watoto waliolazwa katika wodi hiyo leo katika Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Husna Mzunga akipokea fedha kwa ajili ya gharama za kutengeneza kadi mbili za bima ya afya kwa watoto wanaotibiwa katika JKCI kutoka kwa Mratibu wa klabu ya mazoezi ya Xtreme workout bootcamp Felix Chengula baada ya klabu hiyo kufanya usafi katika jengo la watoto, kutoa zawadi kwa watoto na kukabidhi fedha hizo leo katika Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.

Picha na: JKCI

***********************************

Na Mwandishi Wetu – JKCI

WATOTO wawili wanaosubiri matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamekatiwa bima ya afya na mabalozi wa klabu ya mazoezi ya Xtreme Workout Bootcamp.

Mabalozi hao mapema leo wamefanya usafi wa mazingira ya jengo la watoto, wamewatembelea baadhi ya watoto waliolazwa wodini kuwajulia hali na kuwagawia zawadi mbalimbali pamoja na kuwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu.

Akizungumza na waandishi wa habari Mratibu wa shughuli hiyo, Felix Chengule amesema waliona vema kutumia kipindi hiki cha sikukuu ya Eid Al-Adha kutoa walichojaliwa na Mwenyezi Mungu na kuwaonesha upendo watoto wenye uhitaji.

“Kipindi hiki cha sikukuu kibinadamu watu wengi huwa wanajifikiria wenyewe, familia zao na furaha zao wenyewe lakini kuna watu ambao wanakosa vitu hata kidogo kama upendo.

“Ukiacha mahitaji mengine kama malazi, wapo wanaokosa upendo, hivyo tukaona tuje tujitoe kwa wenzetu, badala ya sisi kusubiri kupewa, tutoe tulichojaliwa,” amesema.

Ameongeza “Tumekuja, tumefanya usafi, tumekata bima kwa watoto wawili na kugawa zawadi ikiwamo miswaki na dawa za meno, sabuni za kufulia na kuogea, taulo za kina mama penseli na zawadi nyinginezo.

“Zawadi tulizotoa ni chache, tulitamani kutoa nyingi zaidi hasa bima ya afya, tukipata watu wa kutuunga mkono tutafurahi zaidi, hivi tulivyotoa tumechangishana, tunakaribisha watu wengi zaidi tushirikiane hasa vijana waje tufanye mazoezi pamoja,” alisema.

Akizungumza, Msanii Nguli wa Muziki wa Bongo Flavor kutoka kundi la Wanaume Halisi TMK, Kassim Ally (Sir Juma Nature) ambao ni mabalozi wa Klabu hiyo, amesema wamejifunza mambo mengi kwa kufanya ziara hiyo ya kuwajulia hali wagonjwa.

“Hospitalini ni sawa na kwenda mahakamani ukienda huko ujue tayari ni shida, wasanii wengi wanajisahau hii ni kama ‘primary school’ (shule ya msingi), hapa shida zote zipo mwisho wa siku lazima uje.

“Ni sehemu ya kutakiana faraja, kuna watu wanaumwa hawana msaada, sisi tumekuja hapa leo naamini tumetumwa na Mwenyezi Mungu tuje kuwaona,” amesema Sir Nature.

Ameongeza “Leo ni mwanzo, TMK imerudi, tumeona tuanze hospitalini, tuwaone, tuwajulie hali wenzetu waliolazwa, wanaendeleaje.

Amesema TMK tayari imeanza kuandaa nyimbo mbalimbali ikiwamo zinazotoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya afya. Ipo chini ya ‘carpet’, unajua msanii ukitembea ndiyo unatunga, ukikaa nyumbani huwezi kutunga, tumefika, tumejionea, tutapeleka ujumbe,” amesisitiza.

Kwa upande wake Msanii Amani Temba amewahimiza wasanii wengine na vijana kujenga utamaduni wa kuwakumbuka wagonjwa na wenye mahitaji mengine.

“Wodini, nimewaona watu wana hali ngumu, imenigusa mpaka nimelia, tuwakumbuke wahitaji,” amesema Temba.

Msanii Dollo Francis amesema ni muhimu pia watu kutenga muda wa kumshukuru Mwenyezi Mungu wanapoamka wazima kwani wapo wanaougua, wamelazwa hospitalini.

“Maisha yetu ni mafupi, ukiamka mzima ujue kuna mwingine amelazwa hospitalini, kutoa ni moyo na sisi tumeguswa, tukafika Taasisi ya Moyo na kujitolea tulichojaliwa,” alisema Msanii Dollo

Naye Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Mzunga amewashukuru wanachama wa klabu ya mazoezi ya Xtreme workout bootcamp kwa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kuwakumbuka watoto waliolazwa, kuwajulia hali, pamoja na kuwapatia zawadi.