Home Michezo RAIS DK. MAGUFULI: UWANJA WA TAIFA SASA UTAITWA UWANJA WA MKAPA

RAIS DK. MAGUFULI: UWANJA WA TAIFA SASA UTAITWA UWANJA WA MKAPA

0
…………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Fullshangwe blog
RAIS Dk. John Pombe Magufuli ametangaza rasmi kuwa kuanzia leo na siku zote  Uwanja wa Taifa  utaitwa jina la Uwanja wa Mkapa au Mkapa Stadium kama hatua ya kuenzi jitihada za Rais mstaafu Benjamin Mkapa katika sekta ya michezo.
 
Dk. Magufuli ametoa kauli hiyo leo  wakati akitoa hotuba ya kumuelezea Rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye leo ndio siku ya kumuaga kitaifa baada ya kufariki dunia Julai 24 mwaka huu.
 
Rais Dkt.Magufuli ameelezea  mambo makubwa ambayo yamefanywa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa wakati wa utumishi wake, alitumia nafasi hiyo kuzungumzia jitihada alizofanya katika kuimarisha sekta michezo nchini ambapo hata Uwanja mkubwa wa mpira wa miguu uliopewa jina la Uwanja wa Taifa ulijengwa.
 
Aidha amesema kuwa baada ya kifo cha mzee Mkapa kumekuwepo na maombi mbalimbali ya wadau wa michezo na Watanzania wanaotaka uwanja wa mpira wa Taifa upewe jina la Mkapa,hivyo amekubaliana na maombi hayo.
 
“Mzee Mkapa alisimamia vema suala la michezo, sanaa na burudani.Uwanja wa mpira wa miguu unaofahamika Uwanja wa Taifa ni matokeo ya jitihada hizo, hata hivyo mzee Mkapa hakupenda sana vitu viitwe kwa jina lake. na kwa kuwa leo amelala usingizi najua hawezi kumuadhibu.
 
“Hivyo uwanja huu kuanzia sasa utaitwa Uwanja wa Mkapa au Mkapa Stadium kama  sehemu ya kumuenzi kwa jitihada zake katika michezo.Mzee Mkapa alikuwa mwanamichezo mzuri na alikuwa shabiki wa Yanga.
 
“Ingawa hakuwahi kuniambia ingawa hata Rais mstaafu mzee Jakaya Kikwete amethibitisha hilo kwa kuwa na yeye ni Yanga, sijajua tu mzee Mwinyi yeye ni shabiki wa timu gani,”amesema Rais Magufuli wakati anazungumzia mchango wa mzee Mkapa katika sekta ya michezo.
 
Hata hivyo amesema kuwa  hata COSOTA ambayo inahusika na haki za wasanii katika kunufaika na kazi zao ilianzishwa na mzee Mkapa.