Home Siasa NEC YATANGAZA ZOEZI LA UTOAJI FOMU,YABADILI MAJINA YA MAJIMBO MATATU

NEC YATANGAZA ZOEZI LA UTOAJI FOMU,YABADILI MAJINA YA MAJIMBO MATATU

0

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) ,Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ofisini Kwake jijini Dodoma wakati akitangaza tarehe ya kuchukua fomu na kurejesha huku majimbo matatu yakibadilishwa majina.

………………………………………………………………………

Na. Alex Sonna, Dodoma

Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) imetangaza rasmi ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu kugombea Urais katika uchaguzi mkuu  itakuwa Agosti 5 hadi 25 mwaka huu.

Tamko hilo limetolewa leo na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) ,Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dodoma.

Aidha Jaji Kaijage amesema kuwa fomu za nafasi ya ubunge na udiwani zitatolewa kuanzia Agosti 12 hadi 25 mwaka huu.

Jaji Kaijage amesema fomu kwa ajili ya Urais zitatolewa katika Ofisi za Tume hiyo zilizopo Njendengwa Jijini Dodoma huku nafasi ya ubunge na udiwani zitatilewa katika ofisi za uchaguzi zilizopo katika halmashauri na kata husika.

Pia Jaji Kaijage ameweka wazi kubadilishwa kwa majina ya majimbo ambapo Jimbo la Chilonwa litaitwa Chamwino, Mtera litaitwa Mvumi na Kjito Upele lililopo Mjini Magharibi linaitwa Pangawe.

“Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuwa Tume inaweza mara kwa mara au angalau baada ya miaka 10 kuchunguza mgawanyo wa Jamhuri katika majimbo, ambapo kupitia ibara hiyo imechunguza na haijagawa majimbo mapya bali imebadilisha majina ya majimbo matatu,”amefafanua Jaji Kaijage.

Idadi ya Majimbo ni 264 kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo 214 ni Tanzania bara na 50 yapo Zanzibar huku kata zikiwa ni 3,956.