Home Biashara KUSAYA: KUSITISHA KAZI VIWANDA VYA CHAI SHAMBA LA TUKUYU HAKUKUBALIKI

KUSAYA: KUSITISHA KAZI VIWANDA VYA CHAI SHAMBA LA TUKUYU HAKUKUBALIKI

0

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( suti ya blu) akiwa na mwakilishi wa kampuni ya METL Bw. George Mwamakula (kushoto) wakati akikagua kiwanda cha chai Chivanjee Tukuyu Rungwe leo.Kiwando hicho hicho hakifanyi kazi tangu Aprili mwaka huu na kusababisha kero kwa wakulima.

Kiwanda cha chai Chivanjee kilichopo katika shamba la chai Tukuyu kikiwa kimefungwa bila kufanya kazi. Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya  ameagiza uongozi wa METL kujieleza kwanini umesitisha uzalishaji na ununuzi wa chai ya wakulima kinyume na makubaliano.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (kulia) akiwa kwenye mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mhe. Chalya Nyangindu (kushoto) kuhusu maendeleo ya zao la chai wakati wa ziara yake kutembelea wadau wa zao hilo.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akitazama majani makavu ya chai yaliyotayari kupelekwa sokoni wakati alipokagua kiwanda cha chai Wakulima  (WATCO ) Tukuyu.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Chai Wakulima Bw. Andres de Klerk (kushoto) akikabidhi zawadi ya majani ya chai kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya mara baada ya kutembelea kiwanda hicho Tukuyu wilayani Rungwe

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kushoto) akikabidhi mashine ya kisasa ya kuvunia majani mabichi ya chai kwa mkulima. Mashine hizo zimenunuliwa na Chama cha Ushirika wa Wakulima Wadogo wa Chai wa Rungwe na Busokelo (RUBUTCO-JE) 
( Habari na Picha na Wizara ya Kilimo)

……………………………………………………………………………………..

Serikali imeagiza kampuni ya Mohamed Enteprises (METL) inayomiliki shamba la chai la Tukuyu kutoa maelezo kuhusu matumizi ya shamba hilo ni kwa namna gani wameweza kuliendeleza tangu walipokabidhiwa mwaka 2007 ikiwemo viwanda vya chai.

Akizungumza na uongozi wa kampuni METL leo (15.07.2020) wakati alipotembelea kiwanda cha chai  Chivanjee kilichopo Tukuyu, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alisema hajaridhishwa na sababu za kufungwa kwa viwanda vya chai.

Katibu Mkuu huyo alifanya ziara katika shamba la chai Tukuyu ( Tukuyu Tea Estate) na kujionea kiwanda kikiwa kimesitisha ununuzi wa majani mabichi ya chai na uchakataji toka mwezi Aprili mwaka huu hali inayoathiri wakulima wa Rungwe.

“ Binafsi kama Katibu Mkuu bado sijashawishika kama kampuni ya METL ina jitihada za makusudi za kufungua viwanda  hivi vya Chivanjee na Musekera ili wakulima wa chai wapate soko na nchi ipate mapato yake ” alisema Kusaya. 

Kufuatia hali hiyo ,Katibu Mkuu huyo alitoa maagizo mawili kwa wamiliki wa viwanda hivyo kuwa kabla ya tarehe 30 Julai mwaka huu wawasilishe ofisini kwake Dodoma taarifa ya kina inayo onyesha ukubwa wa eneo, kiasi kilichopandwa chai na ipi mikakati ya kampuni kuendeleza ardhi waliopewa na serikali.

“Katika taarifa hiyo nataka METL muwe wakweli kabla ya kuileta kwangu ili tujirishishe na ukubwa wa shamba hili na matumizi yake” alisisitiza Kusaya.

Kusaya alitaja agizo la pili kuwa METL iwasilishe taarifa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara kabla ya tarehe 30 Julai mwaka huu kuelezea mikakati na mpango kazi wa kufufua viwanda vyote viwili.

Katibu Mkuu huyo aliongeza kusema endapo kampuni METL itapeleka taarifa isiyoshawishi serikali, wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara na ile ya Ardhi watamshauri Rais achukue hatua za kuyatwaa mashamba hayo kwa manufaa ya umma.

“ Kama mtaleta taarifa isiyo na ushawishi kwa serikali, nitaongea na wenzangu wa Viwanda na Ardhi kwenda kumuomba Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili ayatwae mashamba na viwanda vilivyopewa METL kwa mujibu wa sheria ili apatiwe mtu mwingine mwenye uwezo wa kuyaendeleza ” alisema Kusaya.

Kwa upande wake Mwakilishi wa kampuni ya METL George Mwamakula alisema sababu iliyopeleka kiwanda cha Chivanjee kusitisha ununuzi wa chai zilitokana na watu waovu kuiba mashine pamoja na miundombinu ya umeme, mota, vyuma na mfumo wa maji. 

Kuhusu kiwanda cha Musekera kufungwa kampuni ya METL ilisema imepanga kianze kazi mwaka 2022 baada ya ufungaji mitambo mipya na kukarabati miundombinu.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Kusaya alitembelea Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko (ROTCO) cha Tukuyu na kuwasihi waache kugomea kuuza chai yao kwenye kampuni tanzua ya Wakulima Tea Company (WATCO) .

Mgogoro wa ushirika wa wakulima wa chai Rungwe umepelekea wanachama wa ROTCO kutotaka kwenda kuuza majani mabichi kwenye kiwanda cha WATCU wakidai kuwa hawatambui umoja huo na kutaka serikali iwazuie kufanya kazi hadi utatuzi wa mgogoro utakapoisha.

Katibu wa ushirika wa ROTCO Amos Mwakasengo aliomba serikali iagize kampuni ya Mohamed Enteprises kutekeleza mkaba wa mauzo ya chai na ushirika huo kufuatia kusitisha ununuzi wa majani ya chai bila taarifa kunakoathiri wakulima. 

Kusaya alitoa wito kwa wanachama wa ROTCO wakati majadiliano ya kutafuta suluhu yakiendelea wapeleke majani mabichi ya chai kiwanda cha WATCU kuuza na kujipatia kipato badala ya kuacha ikiharibika shambani.

Aidha Kusaya alitembelea Ushirika wa Wakulima Wadogo wa Chai Rungwe na Busokelo ( RUBUTCO-JE) ambapo amewata wakutane na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuona namna watakavyoweza kupata mtaji wa kuanzisha kiwanda cha chai cha ushirika huo ili kuwa na uhakika wa soko la chai .

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo alitembelea pia kiwanda cha parachichi Rungwe (RAC) na kukitaka kisitishe uamuzi wake wa kutonunua parachichi za wakulima kwa kigezo cha kukosa ubora.

Mwisho

Imetolewa na;

 Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

TUKUYU,MBEYA

15.07.2020