Home Mchanganyiko Fedha za Nyongeza Hospitali za Wilaya kwa maelezo- Serikali

Fedha za Nyongeza Hospitali za Wilaya kwa maelezo- Serikali

0

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima, akiongea na Mhandisi Salum Naembe, wakati wa ziara yake katika jengo la Hospitali ya Wilaya. Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima, akiongea na Mhandisi Salum Naembe, wakati wa ziara yake katika jengo la Hospitali ya Wilaya.Naibu Katibu Mkuu akiwa amepigwa na butwaa akishangaa kuona jengo hilo ambalo lipo katika asililia 63 tu ya ujenzi.

***************************************

Na. Atley Kuni-MOROGORO

Serikali imesema haitatoa nyongeza ya fedha kwa Halmashauri zilizoshindwa kukamilisha ujenzi wa majengo saba ya awamu ya kwanza ya Hospitali 67 za Halmashauri za Wilaya kwa Tsh. 1.8 bilioni hadi pale Halmashauri husika zitakapotoa maelezo ya kuelekeweka ni kwa namna gani walitumia fedha hizo zisitoshe.

Kauli hiyo imetolewa kufuatia kutokamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro ambapo ujenzi wake upo kwenye asilimia 63 na majengo kadhaa yakiwa bado hayajakamilika kabisa huku wakiomba nyongeza ya milioni 700.

Akizungumza na timu ya Afya ya Halmashauri hiyo, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Daktari Dorothy Gwajima, alisema inashangaza kuona maeneo mengine ya nchi kwa kutumia kiasi kile kile cha fedha wameweza kufikia asilimia 90 hadi 93 na tayari wenngine wameanza kutoa baadhi ya huduma, lakini kwa hapa Malinyi bado mpo asilimia 63 tu ya ujenzi, hii inashangaza sana.

“Katika hali kama hii na sio kwa Malinyi pekee, Serikali itajiridhisha kwa kina na uzito unaostahili juu ya sababu zipi zilizochangia wengine waweze kukamilisha na wengine kama akina Malinyi washindwe ndipo tuendelee na ajenda inayofuata ikiwemo hatua zote stahiki kwa watakaobainiwa kutumia fedha hizo tofauti na mwongozo na maelekezo”alisema Dkt. Gwajima.

Akizungumza katika eneo la tukio, Mhandisi wa Halmashauri Bw. Salum Naembe amesema, sababu kubwa ya wao kuzidi kiwango kilichokuwa kimekadiriwa hapo awali na Serikali ni eneo hilo kuwa na maji mengi hivyo kuwalazimu kuimarisha zaidi msingi wa majengo hayo.

Serikali katika Mwaka wa fedha 2018/19 kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI, ilitenga kiasi cha Bilioni 1.5 kwa kila Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali mpya 67 za Halmashauri ambapo hadi kufikia Julai,2020 jumla ya Hospitali zipatazo 46 zimekwishaanza kutoa huduma za Wagonjwa wa nje (OPD) zikiwemo huduma za chanjo na kujifungua. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2019/20 Serikali iliongeza Tsh milioni 300 kwa kila Halmashauri hivyo kufanya jumla yote kuwa Tsh 1.8 bilioni kwa kila hospitali inayojengwa.