………………………………………………………………….
Na Woinde Shizza , Arusha
Waziri wa Nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za Mitaa Suleiman Jafo ameagiza wakuu wa Idara zinazohusika katika halmashauri ya Longido kuandika barua ya kueleza kwanini wasichukuliwe hatua kwa kuchelewesha kukamilisha ujenzi wa vituo viwili vya afya vilivyopo katika halamashauri hiyo.
Aidha Mheshimiwa Jafo ametoa agizo hilo leo katika ziara yake ya kukagua miradi ya vituo vya Afya Wilayani Longido mkoani Arusha ambapo alisema hajaridhishwa na utendaji kazi wa miradi hiyo.
“Katika maeneo Mengine tumetoa Bilioni 1.5 na wamekamilisha majengo ya hospitali ya wilaya lakini nyinyi mmepewa hiyo hela mkaongezewa na milioni 300 bado mnadai kuongezewa milioni 400 na hamjakamilisha ujenzi mpo siriazi kweli?Alihoji Mh. Jafo.
Alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt. Juma Mhina kuandika barua ya maelezo pamoja na Idara zote zinazohusika katika kusimamia miradi hiyo huku akimtaka barua hizo kufika ofisini kwake Ijumaa ya wiki hii Julai 10 mwaka huu.
Alisema kutokana na kutoridhishwa na kasi ya utendaji katika halmashauri hiyo ameghairi swala la kujenga kituo chake katika Eneo hilo ambapo alikuwa ameomba fomu ya kutaka kujenga kituo kitakachoshughulikia na mambo ya wizara yake wilayani hapo.
Alimpongeza mkuu wa wilaya hiyo Frank Mwaisumbe kwa kuwachukulia hatua Mhandisi anayesimamia miradi hiyo pamoja na afisa manunuzi wa Halmashauri hiyo kwa kushindwa kutekeleza mradi kwa wakati ikiwa ndio wasimamizi wakuu katika ujenzi huo.
Naye mkuu wa wilaya hiyo alisema wiki mbili zilizopita aliwaweka lokapu watendaji hao kwa kushindwa kusimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati jambo ambalo alisema alilaumiwa na watu wengi huku wakitaka warejee katika majukumu yao.
“Niliwaweka ndani wiki mbili zilizopita lakini nililaumiwa sana na cha ajabu pamoja na kurejea kuendelea na majukumu yao bado uzembe ndo huu unaendelea” alisema.
Ziara ya waziri wa TAMISEMI ililenga vituo viwili vya afya ambapo ni hisipitali ya wilaya ya Longido, inayoendelea kujengwa ikiwa katika hatua za mwisho za ukamilishwaji ambapo zaidi ya bilioni 1.5 zilizotolewa na serikali zimekwishwa kutumika na kingine ni kituo cha Afya Eworendeke kilichopo mpakani mwa Nchi jirani Kenya.