Home Mchanganyiko SERIKALI KUFIKISHA UMEME MGODI WA STAMIGOLD SEPTEMBA

SERIKALI KUFIKISHA UMEME MGODI WA STAMIGOLD SEPTEMBA

0

Kaimu Meneja wa Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold, Mhandisi Rashid Lulamka (aliyenyoosha mkono), akimwonesha Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kushoto kwake), maeneo mbalimbali ya Mgodi huo. Waziri alifanya ziara Mgodini hapo, Julai 6, 2020 kukagua ujenzi wa mradi wa kusafirisha umeme unaotarajiwa kufikishwa eneo hilo Septemba, mwaka huu.

Vibarua wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wakishirikiana kuvuta nguzo katika kijiji cha Kunankwa, Geita, kilicho jirani na Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold. Taswira hii ilichukuliwa wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), Julai 6, 2020 kukagua ujenzi wa mradi wa kusafirisha umeme unaotarajiwa kufikishwa katika Mgodi huo, Septemba mwaka huu.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kulia), akiwa katika ziara ya kazi Julai 6, 2020, kukagua ujenzi wa mradi wa kusafirisha umeme unaotarajiwa kufikishwa katika Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold, uliopo Biharamulo, Septemba mwaka huu.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye miwani – mbele) na Ujumbe wake, akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold. Waziri alitembelea Mgodi huo Julai 6, 2020 kukagua ujenzi wa mradi wa kusafirisha umeme unaotarajiwa kufikishwa katika Mgodi huo, Septemba mwaka huu.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati) akielekeza jambo kwa uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold, alipotembelea Mgodi huo kukagua ujenzi wa mradi wa kusafirisha umeme, Julai 6 mwaka huu.

Sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold. Taswira hii ilichukuliwa Julai 6, 2020 wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), kukagua ujenzi wa mradi wa kusafirisha umeme unaotarajiwa kufikishwa katika Mgodi huo, Septemba mwaka huu.

…………………………………………………………………………………

Veronica Simba – Biharamulo

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha kuwa, ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba, mwaka huu, umeme uwe umefikishwa katika Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold uliopo Biharamulo.

Alitoa maelekezo hayo jana, Julai 6, 2020 alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kupeleka katika Mgodi huo unaomilikiwa na Serikali.

Akizungumza na viongozi wa Mgodi huo, Dkt Kalemani alimshukuru Rais John Magufuli kwa kutenga fedha za kutosha kuweza kutekeleza Mradi huo mkubwa.

“Nataka nitoe taarifa kwenu watu wa Stamigold, kwamba Mheshimiwa Rais ameshatuagiza kutekeleza Mradi huu. Tunazo shilingi bilioni 9.5 kwa ajili ya kuleta umeme hapa.”

Akieleza zaidi, alisema ujenzi wa Mradi huo utakaotumia takribani miezi miwili na nusu, unatekelezwa kwa fedha za ndani kwa asilimia 100.

Aidha, alieleza kuwa umeme utakaopelekwa Mgodini hapo unatolewa eneo la Mpomvu, mkoani Geita, umbali wa takribani kilomita 100 na kwamba ili kuhakikisha umeme huo unakuwa wa uhakika, zitawekwa transfoma mbili katika eneo husika.

Alisema, Serikali imedhamiria uchimbaji wa madini wa aina zote utumie umeme ili uwe na tija hivyo kuwawezesha wachimbaji kulipa tozo stahiki na kutoa gawio kwa Serikali.

Waziri aliutaka uongozi wa Stamigold, baada ya kufikishiwa umeme, kuandaa mapendekezo ya mahitaji yao ya baadaye ya umeme ili Serikali kupitia Wizara ya Nishati ijipange kuwapatia huduma hiyo.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi kwa Waziri, Kaimu Meneja wa Mgodi, Mhandisi Rashid Lulamka, alisema umeme utakapofikishwa Mgodini hapo, utasaidia kuokoa takribani shilingi milioni 700 kwa mwezi ambazo hutumika kununulia mafuta ya kuendeshea mitambo.

“Kwa sasa, tunatumia takribani shilingi bilioni moja kwa mwezi kwa ajili ya kununua mafuta. Tukipata umeme, matarajio yetu ni kushuka kwa kiwango hicho hadi shilingi milioni 300,” alifafanua.

Katika ziara hiyo, Waziri aliambatana na viongozi pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Wizarani, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).