……………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama wamejipanga kudhibiti vitendo vya kitapeli kwa kujifanya wapo karibu na viongozi wakuu wa kitaifa wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa CCM.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (SAC) Gilles Muroto amesema wamejipanga kudhibiti vitendo hivyo ili mkutano huo ufanyike kwa usalama na amani bila vitendo vya kitapeli kutamalaki.
“Jeshi limejipanga kuhakikisha yeyote atakayejaribu kufanya utapeli wa kujifanya wapo karibu na viongozi wakuu wa kitaifa hawataondoka Dodoma wajipange kubakia na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema
Katika mkutano huo Mkuu wa CCM utakaofanyika kati ya Julai 7 hadi 12, mwaka huu, utachagua na kupitisha wagombea wa nafasi ya Rais Tanzania Bara na Zanzibar kwa tiketi ya CCM.
Muroto amesema mkutano huo unaotarajiwa kuwa na wajumbe zaidi ya 3,000 hatapenda kuwaona watu wanaotaka kutenda vitendo vya kitapeli kwa kujifanya wapo karibu na viongozi hao.
Amesema uzoefu unaonesha kwamba katika mikutano kama hiyo wamekuwa wakihudhuria watu mbalimbali wakiwemo wapambe wa wagombea, familia za wagombea, wapiga debe, wajasiliamali lakini pia wanakuwepo watu wabaya ambao wanatumia fursa hiyo kutekeleza azma yao ya kihalifu.
Muroto amesema makundi hayo ambayo yanapanga kufanya vitendo vya kihalifu wasije wakaingia katika mtego ambao hawakutarajia, jeshi hilo limejiandaa kikamilifu kulinda vitendo hivyo vya kitapeli visitokee.
Vilevile, Jeshi la Polisi limefanya oporesheni za kutafuta wezi wa magari na limewakamata watuhumiwa wawili ambao wamekiri kufanya matukio mbalimbali ya wizi na unyang’anyi wa magari ya nchini na yale ya kutoka nje sambamba na kuwapa dawa ya kulevya abiria katika mabasi kupitia biskuti.
Pia katika oporesheni hiyo wamekamata silaha mbili aina ya pistol na risasi 14 inaomilikiwa na Jumbe Kamugisha (46).
Kamugisha ni mkazi wa Chanika Msongola wa Jijini Dar es Salaam akiwa na vidonge 124 aina ya Rolvan na pakti moja ya biskuti wanazotumia wahalifu kuwalewesha abiria kwenye mabasi.
Silaha nyingine iliyokamatwa ni aina ya browning pamoja na risasi 15 inayomilikiwa na George Semtego (36). Semtego ni Mbondei, mfanyabiashara, mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Muroto amesema silaha hizo zinamilikiwa kihahali lakini zimekuwa zinatumika katika matukio ya kihalifu ambapo Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa hawalipii lakini pia hazikuhakikiwa na kupewa namba za silaha za hapa nchini.
Ametoa wito kwa wanaomiliki silaha na kutumia kitendo cha uhalifu wote kuchukuliwa hatua na kushtakiwa mahakamani.