Home Mchanganyiko Pongezi kwa Mhe. John Pombe Magufuli kwa Tanzania kuingia katika Orodha ya...

Pongezi kwa Mhe. John Pombe Magufuli kwa Tanzania kuingia katika Orodha ya Nchi za Uchumi wa Kati

0

Julai 1, 2020 Benki ya Dunia iliutangazia ulimwengu kuwa imeiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati, hatua iliyojiri miaka mitano kabla ya muda uliopangwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2025.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inatoa pongezi za dhati kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mafanikio haya.

Ni dhahiri kuwa hatua hii imefikiwa mapema hivi kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano tangu iingie madarakani mwaka 2015. Jitihada hizi zimechochea ukuaji wa pato la taifa, zimeshusha mfumuko wa bei, zimevutia uwekezaji kutoka nje, zimepunguza ukosefu wa ajira na kuendeleza sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Miongoni mwa jitihada hizo, zilizofanyika chini ya uongozi shupavu na makini wa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ambazo tunaamini zimewezesha Benki ya Dunia kuitangaza Tanzania kuwa nchi ya  kipato cha kati ni mafanikio ambayo Tanzania imeyapata katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati iliyotoa ajira kwa wananchi wengi.

 

Maboresho ya miundombinu ya barabara, ikiwemo barabara zenye kiwango cha lami ambazo zinaunganisha mikoa na kuwezesha  watanzania kusafirisha mazao kutoka mashambani hadi kwa walaji, yamewafaidisha wananchi wa kawaida, wafanyabiashara wadogo wadogo, wa kati, wakubwa, wakulima na wafugaji.

 

Aidha, miradi ya usambazaji umeme inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na uwepo wa umeme wa uhakika siyo tu imewezesha watanzania wengi kuwa na nishati ya umeme wa uhakika majumbani, bali pia imewezesha wafanyabiashara wa ngazi mbalimbali kufanya biashara na kuongeza vipato.

 

Jitihada nyingine zilizochochea nchi yetu kuingia katika uchumi wa kati ni utekelezwaji wa azma ya kujitegemea, ukusanyaji wa kodi, nidhamu katika matumizi, uzingatiaji wa maadili na miiko ya uongozi, kuwekeza kwenye miradi inayokuza uchumi, maendeleo ya watu na sekta binafsi yenye tija. Hatua hizi zimeweza kuwafikisha watanzania kupata huduma kama vile upatikanaji wa matibabu pamoja na dawa, na utoaji wa elimu bure kwa watanzania.

Kutokana na uongozi imara wa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, udhibiti wa fedha za umma umeongezeka; pia Tanzania imeshuhudia ukuaji wa sekta ya viwanda, ambapo zaidi ya viwanda 8,000 vimeanzishwa katika kipindi cha miaka mitano, ukilinganisha na viwanda 60 tangu uhuru. Hatua hizi zimepelekea uchumi wa nchi kuimarika zaidi.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inawaomba watanzania kuendelea kulinda na kuthamini hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kulinda haki za binadamu na kudumisha amani na utulivu uliopo pamoja na kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora ambayo ni chachu ya amani, utulivu na usalama wa Taifa letu.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inatambua kuwa hatua hii kubwa ya nchi yetu kuingia katika orodha ya nchi za uchumi wa kati imetokana na jitihada makini za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia na kuratibu mageuzi makubwa kiuchumi, na hivyo kupanua haki na huduma za kijamii na kiuchumi kwa watanzania wote.

Tume inatoa wito kwa viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali kuendelea kutumia mamlaka zao kwa kuzingatia uwazi, uwajibikaji, ushirikishaji wa watu, ufanisi, tija, uadilifu, usawa na utawala wa sheria. Tume inaamini kuwa uzingatiaji wa misingi hii ya utawala bora umekuwa na mchango mkubwa katika kuiwezesha Tanzania kupiga hatua ya kuingia katika uchumi wa kati.