Home Mchanganyiko SERIKALI YASHAURIWA KUGHARAMIA MATIBABU YA FISTULA YA UZAZI

SERIKALI YASHAURIWA KUGHARAMIA MATIBABU YA FISTULA YA UZAZI

0
Mratibu wa Shirika la MAPERECE la wilayani Magu, Lativas John Bifandimu akitoa mada kwa Mabalozi wa Fistula wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yanayotolewa na shirika hilo ambapo yalifanyika jijini Mwanza.

Daktari Kiongozi wa Wodi ya Vizazi na Uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) Dk. Reolvin Elishaphat akitoa mada ya ugonjwa wa Fistula ya Uzazi kwa Mabalozi wa Fistula wilayani Nyamagana.

Washiriki wa mafunzo ya kujenga uwezo wa Mabalozi wa fistula Wiaya ya Nyamagana wakimsikiliza Mratibu wa Mafunzo hayo Lavitas John Bifandimu wa shirika MAPERECE.
Picha zote na Baltazar Mashaka
………………………………………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza

SERIKALI imeshauriwa kugharamia matibabu ya Fistula ya Uzazi, kuboresha huduma za afya ya uzazi na miundombinu kwenye hospitali na vituo vinavyotoa huduma za dharura ili kuwasaidia wanawake wanaokabiliwa na ugonjwa huo. 

Ushauri huo ulitolewa jana kwa nyakati tofauti jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Shirika la MAPARECE, Julius Mwongela na Kiongozi wa Wodi ya Magonjwa ya Vizazi na Uzazi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) Dk. Reolvin Elishaphat, walipohojiwa na gazeti hili wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Mabalozi wa Fistula wilayani Nyamagana.

 Walisema tatizo la ugonjwa wa fistula ya uzazi ni kubwa kwenye jamii hasa vijijini kutokana na changamoto mbalimbali za ukosefu wa elimu, uchumi na huduma duni za afya ya uzazi zinazotolewa hivyo Wizara ya Afya ilibebe na kuliweka kwenye Afya ya Mama na Mtoto tatizo hilo ili wanawake hao watambuliwe na kutibiwa bure.

“Tunachokifanya kuhusu fistula ni kui engage  serikali kulibeba suala hilo liingizwe kwenye afya ya Mama na Mtoto maana wanawake wenye tatizo hilo wametengwa wakati yote yanahusu uzazi.Wizara ikilichukua na kulitambua mwishowe watatambuliwa na kutibiwa bure lakini kwa ilivyo sasa ni kuwabeza wanawake wenye fistula,”alisema Mwongela.

Naye Dk. Elishaphat alisema fistula ya uzazi inachangiwa na changamoto ya uelewa mdogo wa jamii na  mitizamo hasi, huduma duni za afya ya uzazi wakati wa kujifungua,umbali mrefu kutoka vituo vya kutolea huduma au hospitali, matatizo ya kifamilia na kiuchumi, miundombinu mibovu ya usafiri hasa visiwani ni tatizo na jiografia ya kila eneo.

“Takwimu za hospitali ya Bugando zinaonyesha tangu Juni mwaka jana hadi Februari 2020 tulipokea wagonjwa 34 ambapo Wilaya ya Nyamagana walikuwa 10, hivyo utaona namba na ukubwa wa tatizo lilivyo.Tunatambua juhudi za Rais John Magufuli za kujenga vituo vya afya, serikali sasa iboreshe sehemu zinazotoa huduma za dharura ili kutokomeza fistula,”alisema Dk. Elishphat.

Kiongozi huyo wa Wodi ya Magonjwa na Vizazi na Uzazi alisema bajeti ya kumhudumia mgonjwa mmoja wa fistula kwa mwezi ni sh.milioni 40 huku upasuaji ukigharamu sh. 800,000 na kushauri  ni vema serikali ikalibeba gharama hizo ili kuwaokoa wanawake wenye fistula kuliko gharama hizo kubebwa na mfadhili ikitokea akajitoa wengi watapoteza maisha.

Alisema wanatoa elimu kwa watoa huduma za afya za msingi vijijini na mijini ( Mabalozi wa Fistula) ili jamii ifahamu ukubwa wa tatizo hilo, dalili na madhara yake, matibabu yanapatikana wapi na kuondoa dhana kuwa fistula ya uzazi inasababishwa na kulogwa ama kujamiiana na wanaume wengi ambapo ugonjwa huo unatibika.

Baadhi ya wanawake waliokuwa wakiugua fistula baada ya kujifungua Remmy Emmanuel, mkazi wa Kijiji cha Lugeye wilayani Magu na Asteria Mabirika, mkazi wa Kijiji cha Chananja, Kata ya Mbarika, Wilaya ya Misungwi walisema afya zao zimeimarika na hawatokwi na mkojo tena baada ya kutibiwa na  kupona.

Alisema kuwa alianza kutokwa na mkojo mfululizo bila kujitambua baada ya siku tatu tangu aliporuhusiwa kurudi nyumbani na baada ya kupata tatizo hilo mumewe alimkimbia na kumtekeleza pamoja na watoto wanne, akauza mazao yote na kuoa mwanamke mwingine.

 “Nashukuru MAPERECE kuniibua, tatizo la kutokwa mkojo mfululizo nililipata baada ya kujifungua, nilikaa kwenye uchungu kwa wiki nzima bila kupata msaada wa wauguzi.Muuguzi alinitukana nilipoomba msaada hadi nikakata tamaa ya kuishi na hata siku najifungua niliwekewa vyuma mtoto akatoka kwa kuvutwa,nikapoteza fahamu ,”alisema Remmy.

 Naye Asteria alisema fistula aliishi na ugonjwa huo kwa miaka mitatu hali ambayo ilisasababisha akimbiwe na wanaume wawili tofauti alioolewa nao kabla na baada ya kupata ugonjwa huo ambao aliamini amelogwa. 

Alieleza kuwa baada ya kupata fistula alihangaika hospitali za Sumve na Bugando na kuambiwa hauna tiba ambapo alikwenda kwa mganga wa kienyeji ambaye alikuwa akimpa tiba ya kukalia dawa kwenye kiti lakini bado aliendelea kutokwa na mkojo. 

“Nilichukuliwa na MAPERECE hadi Bugando na kupimwa ambapo niliambiwa nina tundu kubwa ambalo linasababisha mkojo kupita bila kutambua.Nilifanyiwa upasuaji leo mwezi wa nne, niwashauri wanawake wenye ugonjwa huo mbaya lakini unatibiwa hivyo wasione aibu wajitokeze fistula inatibiwa,”alisema Asteria.

Aidha, Mratibu wa Afya ya Uzazi Wilaya ya Nyamagana,Bertha Yohana kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Jiji, Juma Mfanga, alisema tatizo la fistula halikupewa kipaumbele kuwa mama anaweza kujifungua na kupata tatizo ama na kikwazo chochote cha uzazi na kushauri elimu inayotolewa kwa mabalozi wa fistula ilete mabadiliko chanya kwenye jamii ili kuibua wagonjwa wapya