Home Mchanganyiko SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA MFUMO WA HUDUMA KWA WATEJA KATIKA MAMLAKA ZA SERIKALI...

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA MFUMO WA HUDUMA KWA WATEJA KATIKA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA.

0

   

********************************

Na. Majid Abdulkarim, Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia maswala ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito na kuwasisitiza watumiaji wote wa huduma za afya nchini katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za halmashauri kutumia namba za huduma kwa wateja zilizopo katika vituo hivyo ili kuwasilisha kero zao mahali sahihi na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Dkt. Gwajima ametoa wito huo leo Jijini Dar es Salaama akiwa  katika ziara ya kikazi ya kukagua uimarishaji mfumo wa huduma kwa wateja katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na Hospitali ya Sinza Palestina .

Aidha Dkt Gwajima amesema, mahala sahihi pa kuripoti Kero za Wateja wakati wa kupata huduma ni kwa Mganga Mkuu wa Kituo, Mganga Mkuu wa Halmashauri, Mganga Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI na ikishindikana hapo Wizara ya Afya.

“ Ili kurahisisha kero hizo kufika kwa wakati  kila kituo cha kutolea huduma za afya (zahanati, kituo cha afya na hospitali ya Halmashauri) sasa kinatekeleza kuimarisha mfumo mzima wa huduma kwa wateja kwa kutumia utaratibu wa kuweka namba za simu kwenye enao la wazi linaloonekana hususani pale wanapokaa wateja kusubiria huduma hivyo, wateja wahakikishe wanapata namba hizo na kuzitumia ili kusaidiwa kwa wakati”, amesisitiza Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima amesema kuwa Wito huo  umekuja baada ya kubaini uwepo wa matukio ya baadhi ya watumiaji wa huduma za afya katika baadhi ya vituo kulalamikia kero walizokutana nazo wakati wa kupata huduma za afya huku muda mrefu ukiwa umepita hivyo, kukosa fursa ya kupata ufumbuzi kwa wakati.

Lakini pia Dkt Gwajima amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri zote nchini ndani ya siku saba kuhakikisha mfumo huu unaimarishwa mara moja na taarifa zinawafikia wananchi wote waanaotumia huduma katika maeneo husika.

Kwa kuongezea Dkt. Gwajima amesema kuwa, kila zahanati, kituo cha afya na hospitali ya Halmashauri lazima iwe na bango kubwa lenye kuonesha namba maalumu ya simu ya kituo kwa ajili ya kushughulikia kero za wateja wanaokuja kupata huduma za afya vilevile, namba ya Mganga Mfawidhi wa Kituo husika, namba ya Mganga Mkuu wa Halmashauri, Mganga Mkuu wa Mkoa, namba za Ofisi ya Rais TAMISEMI na namba ya Kituo maalumu cha Simu (Call Centre) cha Wizara ya Afya ambayo ni 199.

“Na sisi kama Ofisi ya Rais TAMISEMI leo tunatangaza namba maalumu ya kupokea Kero na Pongezi kutoka kwa wateja juu ya utoaji huduma za afya katika hospitali zetu za ngazi ya afya ya msingi na namba hiyo ni 0734124191. Hivyo, iwapo Mteja utakuwa na Kero na hujapata msaada ngazi ya kituo, mganga mkuu wa halmashauri na mkoa basi usiondoke na kero yako bali haraka tuma ujumbe juu ya kero hiyo ukieleza uko Halmashauri gani na Kituo gani na sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI tutakupigia na kuchukua hatua stahiki za kupata ufumbuzi juu ya kero hiyo kwa wakati sahihi” ameeleza Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima amebainisha kuwa lengo la kuimarisha huduma kwa Wateja ni kutatua kero zao kwa wakati na kuhakikisha kila mwananchi anayefika kwenye kituo cha huduma za afya ngazi ya msingi anafurahia huduma hizo na haondoki huku moyoni akiwa na manung’uniko yasiyo ya lazima.

Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima amewapongeza wataalamu wa sekta ya afya nchini kwa kupokea kwa uzalendo na kutekeleza kwa vitendo mwelekeo wa kupambana na kudhibiti ugonjwa wa Covid 19 kupitia maono makubwa ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuwa.

“tuwe wabunifu na tupigane vita hii bila hofu na kwa kuzingatia mazingira mahsusi ya nchi yetu, Kupitia maono haya Covid 19 imedhibitiwa mapema sana na Tanzania imeandika historia duniani juu ya mbinu za ubunifu na uzalendo juu ya mapambano haya”ameeleza Dkt.Gwajima.

Dkt Gwajima amesema, jukumu liliko mbele ya wataalamu wa huduma za afya nchini  ni kuimarisha utekelezaji wa miongozo ya kinga kwa ujumla ili uzoefu uliopatikana uendelee kwa ajili ya kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza na kuipungizia Serikali mzigo wa kuhudumia wagonjwa ambao wangeepuka kuugua magonjwa hayo iwapo wangepata elimu ya kujikinga na kutekeleza kwa vitendo mfano kunawa mikono.

 “tusiache kuendeleza hizi mbinu za usafi zinazolenga kujikinga na magonjwa ya kuambukiza hususan kunawa mikono ili tudhibiti na kutokomeza kabisa magonjwa hayo yakiwemo kipindupindu na magonjwa yote ya tumbo yatokanayo na kula vyakula kupitia mikono isiyo safi” amesisitiza Dkt. Gwajima.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Dkt.Rashid Mfaume amesema kuwa yeye kwa kushirikiana na watendaji wenzake ndani ya mkoa wa Dar es salaam ndani ya siku saba watakuwa wametekeleza agizo la kuhakikisha kunakuwa na mfumo na utaratibu wa kupokea na kushughulikia kero za wateja kwenye vituo vya huduma za afya kwa kutengeneza mabango makubwa yenye ubora wa kipekee yakionesha namba za simu zilizoelekezwa ili wananchi wafahamu na kuzitumia kwa wakati.

Huku Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dkt. Delila Moshi akiahidi kutekeleza agizo hilo haraka sana kwa kusambaza mabango hayo kwenye maeneo yote muhimu waliko wateja huku akitumia mfumo wa matangazo ya sauti kuwafikia wateja wengi zaidi.

Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Dharura na Maafa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Christopher Mzava ametoa wito kwa wahudumu wa afya kuendelea kushirikiana kwa karibu na wateja ili kuweka mazingira mazuri ya kupokea mrejesho juu ya huduma wanazotoa kwa ajili ya kufanya maboresho zaidi.