Home Mchanganyiko MWAKALINGA AMPA SIKU SABA MKANDARASI BARABARA YA RUDEWA-KILOSA

MWAKALINGA AMPA SIKU SABA MKANDARASI BARABARA YA RUDEWA-KILOSA

0

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli pamoja na viongozi mbalimbali wakifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24 mkoani Morogoro kwa kiwango cha lami.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga (kulia) akijadiliana jambo na Waziri wa Nishati Mhe. Dk. Medard Kalemani mara baada ya hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24 mkoani Morogoro kwa kiwango cha lami.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga (kulia) akiwa katika mkutano na wakandarasi wa Umoja-Kilosa JV wanaojenga barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24 mkoani Morogoro.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24 mkoani Morogoro ambayo inayoendelea na ujenzi.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24 mkoani Morogoro inayoendelea na ujenzi.

KUFUATIA agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli la kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24 mkoani Morogoro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga amempa siku saba mkandarasi (Umoja-Kilosa JV ), kuja na mpango mkakati mpya unaotekelezeka kwa haraka.
Katika hafla ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa na muunganiko wa wakandarasi wazawa saba Umoja-Kilosa JV Rais Dakta, Magufuli licha ya kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo ametoa mwezi mmoja kwa mkandarasi huyo kufanya mabadiliko chanya kama anataka kuendelea na ujenzi wa mradi huo.
Akizungumza katika kikao cha dharura kati ya Katibu Mkuu Mwakalinga, Wakala wa Barabara nchini TANROADS na mkandarasi Umoja-Kilosa JV Arch. Mwakalinga amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa haraka na ubora uliokusudiwa ili kuiwezesha Serikali kuwa na imani na wakandarasi wazawa.
“Hakikisheni mnajenga imani kwa Serikali yenu ili iwaamini na hivyo muweze kupata miradi mingi ya ujenzi hapa nchini na hivyo kukuza uchumi wa nchi na ajira kwa wazalendo,” amesisitiza Katibu Mkuu Mwakalinga.
Amesema nia ya Serikali ni kuwawezesha wakandarasi wazawa kuwa na uwezo na mtaji na hivyo kujenga miradi mingi ya ujenzi ili fedha nyingi inayolipwa kwa wakandarasi kubaki nchini na kuhuisha uchumi na kukuza ajira za Watanzania.
“Kuungana, uaminifu, uzalendo na kuchapakazi kwa bidii, kutaiwezesha Serikali kutoa miradi mingi ya ujenzi kwa wakandarasi wazawa na hivyo kuwajengea uwezo wa kimtaji, utaalam na uzoefu na kuongeza ajira kwa watanzania”, amebainisha.

Barabara ya Rudewa-Kilosa KM 24, ni sehemu ya barabara ya Dumila-Kilosa-Mikumi yenye urefu wa Km 142, barabara hiyo inayotarajiwa kukamilika Januari mwakani itakapokamilika itaunganisha kwa njia fupi mikoa ya Tanga,Morogoro na Iringa bila kupita mbuga ya wanyama ya Mikumi na hivyo kupunguza ajali katika mbuga hiyo.