Home Mchanganyiko KAMATI YA MAADILI YAZINDULIWA MLOGANZILA

KAMATI YA MAADILI YAZINDULIWA MLOGANZILA

0

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Charles Majinge akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati ya maadili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika uzinduzi

Prof. Majinge na viongozi wakuu wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya maadili ya MNH-Upanga na Mloganzila.

Katibu Kanda ya Mashariki, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bi. Getrude Cyriacus akiwasilisha mada ya maadili kwa watumishi wa umma kwa wajumbe wa kamati ya maadili.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi huo.

************************************

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila yazindua kamati ya maadili ikiwa ni mwitikio wa utaratibu uliowekwa na Serikali unaozitaka idara za Serikali na taasisi za umma kusimamia na kudhibiti uadilifu.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Charles Majinge wakati akizindua kamati hiyo ambayo itakuwa chini ya uongozi (Executive Management Sub-committee) ikihusika na utekelezaji na mikakati ya kudhibiti uadilifu na kuwasilisha taarifa zake katika kamati ya uongozi kwa hatua zaidi.

“Serikali inapambana ili kuzuia rushwa kutokana na kuporomoka kwa maadili ya watoa huduma inayosababishwa na kukosa nia ya kufanya kazi kwa kufuata miongozo mbalimbali iliyowekwa badala yake kuweka tamaa ya fedha mbele na kupelekea kuharibu uzuri wa huduma za afya zinazotolewa kwa umma” amesema Prof. Majinge.

Prof. Majinge ametaja kuwa suala la maadili ni jambo pana linahusisha malezi kuanzia mtoto anapozaliwa hadi anakuwa mtu mzima na hivyo ni jukumu la wazazi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wanalelewa katika maadili mema ili kujenga jamii iliyo bora.

“Malezi bora ndiyo yanayojenga jamii bora na ili tuweze kufikia hatua ya kutokomeza rushwa kabisa katika jamii yetu ni lazima tuhakikishe watoto wanalelewa katika maadili mema kwani tunayodhamana ya kuwahudumia watanzania kwa haki na sio kwa lengo la kupata zawadi” amesema Prof. Majinge.

Awali, akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru amesema kamati hiyo itasaidia katika kusimamia jukumu zima la kutoa huduma bora na kusimamia utendaji wa hospitali kwa kuhakikisha miongozo yote ya Serikali inafuatwa.

Kwa upande wake mtoa mada katika uzinduzi huo, Katibu Kanda ya Mashariki, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bi. Getrude Cyriacus amewataka watumishi wote wa umma kuzingatia maadili, weledi, sheria na kanuni zinazosimamia utumishi wa umma ili kufikia malengo ya kutoa huduma bora kwa wananchi wote hasa wanyonge kama dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inavyoelekeza.