Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga Bi. Specioza Owure akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo ambapo amewaomba wafanyabiashara waendelee kutoa ushirikiano kwa maafisa wa TRA wanaofanya kampeni hiyo.
Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Julius Mjenga (kulia) akimuelimisha Mfanyabiashara wa jijini Tanga wakati wa Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani humo. Kushoto ni Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka hiyo Bi. Ernesta Shirima.
Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Julieth Shehiza akimuelimisha Mfanyabiashara wa jijini Tanga wakati wa Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Julieth Shehiza akikagua cheti cha Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) cha Mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi wa jijini Tanga wakati wa Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Julius Mjenga akichukua taarifa za mfanyabiashara wa vipuli vya pikipiki wa jijini Tanga wakati wa Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani humo.
PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO.
********************************
Na Mwandishi wetu
Tanga
WAFANYABIASHARA wa Mkoa wa Tanga, wamesema hawaoni shida ya kulipa kodi baada ya kuona utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kupitia kodi zao.
Wafanyabiashara hao wametoa kauli hiyo, wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayofanywa na maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka Makao Makuu wakishirikiana na maafisa wa TRA mkoa wa Tanga.
Maafisa hao waliwatembelea wafanyabiashara hao kwenye maduka yao yaliyopo barabara za namba jijini Tanga kwa lengo la kuwaelimisha na kuwakumbusha kulipa kodi kwa wakati.
Sambamba na hilo, maafisa hao pia waliweza kusikiliza kero zinazowakabili wafanyabiashara hao na kusikiliza maoni yao kama mpango wa kutengeneza mazingira rafiki kati yao na TRA.
Thabiti Salimu ni mfanyabiashara wa Ukwaju wa jumla na rejareja wa eneo la barabara za namba ambaye alisema kuwa, atamshangaa mfanyabiashara anayekwepa kulipa kodi hususani katika kipindi hiki ambacho wameona miradi mingi ikitekelezwa kupitia kodi zao.
“Rais Dkt. Magufuli anatumia kodi zetu vizuri, tunaona utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo hivyo lazima tuendelee kulipa kodi la sivyo kazi ya utekelezaji wa miradi hii itakwama,” alisema Salimu.
Salimu amepongeza mpango ulioanzishwa na mamlaka hiyo wa kuwatembelea wafanyabiashara na kuwasikiliza akisema ni mpango mzuri ambao unapaswa uendelee kutokana na umuhimu wake kwa ustawi wa mlipakodi.
Kwa upande wake Dina Mbenu, mfanyabiashara wa vipuli vya pikipiki alisema kuwa, ikiwa wafanyabiashara watakwepa kulipa kodi watasababisha madhara ya kiuchumi na kuathiri jitihada za Mh. Raisi za kuboresha miundombinu ikiwemo barabara.
Mbenu alisema hatua ya maafisa wa TRA kuwatembelea kwenye maduka yao kwa lengo la kuwahamasisha kulipa kodi na kusikiliza kero na maoni yao inawasaidia kutopoteza muda kwenye ofisi za TRA wakisubiri kuhudumiwa.
Naye Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi Julius Mjenga alisema zoezi la kuwatembelea wafanyabiashara ni endelevu na kabla ya kufanyika Tanga, zoezi hilo limeshafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Morogoro.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kutoa elimu ya kodi, kuwakumbusha wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati, kusikiliza maoni yao pamoja na changamoto kwa ajili ya kuzitatua.
Kwa upande wake Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Specioza Owure, aliwaomba wafanyabiashara kuunga mkono zoezi linalofanywa na maafisa wa TRA la utoaji elimu ya kodi, kusikiliza maoni na changamoto zao kwa kuwa zoezi hilo linalenga kuboresha huduma kwa mlipakodi.
“Niwaombe wafanyabiashara wote mkiwaona maafisa wanatembelea, msifunge maduka, wapokeeni na kuwapa ushirikiano kwa kuwa wanalenga kuwaelimisha na kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye biashara zenu ambazo kwa pamoja tunaweza kuzitafutia ufumbuzi,” alisema Owure.
Kwa mujibu wa Owure, maafisa hao wakiwa mkoani Tanga watafanya zoezi hilo mpaka tarehe 30 Juni, 2020 lengo ikiwa ni kutaka kuwafikia wafanyabiashara wengi mkoani hapa.