Home Mchanganyiko NDEGE ZA ABIRIA 200 KUTUA KIWANJA CHA DODOMA

NDEGE ZA ABIRIA 200 KUTUA KIWANJA CHA DODOMA

0

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, Bi. Bertha Bankwa (kulia), wakati Waziri huyo alipokagua maendeleo ya upanuzi wa kiwanja hicho mkoani Dodoma.

Meneja wa Wakala Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, akitoa maelezo kwa Waziri wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, kuhusu hatua iliyofikiwa ya upanuzi wa Kiwanja ch Ndege cha Dodoma, wakati Waziri huyo alipokagua maendeleo ya ujenzi wake.

Kazi ya upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Dodoma ikiendelea. Mradi huo umefikia asilimia 30 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

Mafundi wa Kampuni ya CHICO wakiendelea na kazi ya upimaji katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma. Mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.5.

*****************************

Serikali imesema kukamilika kwa upanuzi wa mita 250 katika kiwanja cha ndege cha Dodoma kutaruhusu ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 aina ya Airbus kuruka na kutua kiwanjani hapo.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya upanuzi huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema lengo la upanuzi huo ni kuruhusu ndege nyingi zaidi kutoa huduma kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani.

“Kiwanja hiki kiliongezwa urefu lakini mahitaji yaliyopo sasa ni makubwa, tumelazimika kuongeza tena urefu ili kukidhi mahitaji kwani idadi ya watu inaongezeka kila siku kwa kuwa Dodoma ni Makao Makuu sasa ya Serikali”, amesema Waziri Mhandisi Kamwelwe.

Waziri Mhandisi Kamwelwe amesema pamoja na upanuzi wa uwanja huo, Serikali imetangaza zabuni kwa ajili ya kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Msalato na zabuni hizo zitafunguliwa mwezi Julai ili kuendelea na taratibu za ujenzi.

Aidha, Waziri Kamwelwe ameongeza kuwa pamoja na changamoto ya ugonjwa wa Corona (COVID 19) kuchangia ucheleweshaji wa ufunguaji na uchambuaji wa zabuni, Serikali inaendelea kuandaa mazingira ili mradi huo uanze.

Katika hatua nyingine Waziri Mhandisi Kamwelewe amesema Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma (ringroad) zenye urefu wa kilometa 112 ambao utakuwa na wakandarasi watatu.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, amemuhakikishia Waziri  kuwa ujenzi huo unakamilika kwa wakati, viwango na kuzingatia thamani ya fedha.

Mhandisi Chimagu ameongeza kuwa pamoja na kuwa kulikuwa na changamoto ya maji mengi, lakini wahandisi walipambana na kukabiliana na maji hayo kwa kuanza na uwekaji wa mawe makubwa kabla ya tabaka la kwanza ili kuimarisha barabara ya kuruka na kutua ndege. 

Mradi wa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, unafanywa na Kampuni ya CHICCO, na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.5.