Home Michezo SERIKALI YAZUIA MASHABIKI KUINGIA KATIKA MECHI ZOTE ZA NYUMBANI ZA JKT TANZANIA...

SERIKALI YAZUIA MASHABIKI KUINGIA KATIKA MECHI ZOTE ZA NYUMBANI ZA JKT TANZANIA FC 

0

……………………………………………………………………………………

Serikali imezuia Timu ya JKT Tanzania FC kucheza na mashabiki kwa mechi zake zote zilizosalia kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Jamhuri, Dodoma, kutokana na kukiukwa kwa Mwongozo wa Afya Michezoni wakati wa mchezo kati ya timu hiyo na Young Africans ya Dar es Salaam. 

Katika mchezo huo na. 288 uliochezwa jana Jumatano, Juni 17, 2020, mashabiki walijazana uwanjani na kukaa bila kuzingatia Kanuni ya 2.0.2 (iii) inayosisitiza kuachiana mita moja. Pamoja na hatua mbalimbalia za kiafya kuzingatiwa, uchunguzi umebaini kuwa wawakilishi wa timu mwenyeji ambao ndio waliokuwa wakidhibiti mageti hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo na badala yake waliruhusu mashabiki wenye tiketi na wasio na tiketi kuingia uwanjani hovyo na kuharibu mpangilio wa ukaaji ambao mpaka saa nane mchana ulikuwa umezingatiwa vyema. 

Hatua hii inalenga kuvikumbusha vilabu mwenyeji, wasimamizi wa michezo na wadau wengine kote nchini kuendelea kusimamia kikamilifu Mwongozo wa Afya na taratibu nyingine michezoni hadi hapo Serikali itakapojiridhisha kuwa Ugonjwa wa Covid-19 umekwisha kabisa hapa nchini. Hatua hizi zinalenga kuwalinda wananchi, wachezaji wenyewe, viongozi na watanzania kwa ujumla. 

Serikali itaendelea kuchukua hatua kali zaidi kwa wale wote watakaoendelea kukaidi miongozo mbalimbali inayotolewa wakati huu wa changamoto za ugonjwa wa Covid-19 unaotokana na Virusi vya Corona.