Home Siasa KANALI LUBINGA AWAONYA WABEBA MABEGI YA WAGOMBEA

KANALI LUBINGA AWAONYA WABEBA MABEGI YA WAGOMBEA

0

*****************************

KATIBU wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga amewaonya viongozi na watendaji wa Chama kuacha kubeba mabegi ya wagombea wakati huu ambapo chama cha mapinduzi kinaelekea katika chaguzi zake za ndani.

Kanali Lubinga ametoa onyo hilo leo wakati akizungumza na viongozi wa CCM Wilaya zote Mkoani Geita katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Geita.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na wakuu wa Wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa.

” Nashukuru tayari Katibu Mkuu wa Chama amewaonya wale wabeba mabegi ya wagombea, na amesema ataiambia Serikali iwafukuze…” Alisema Kanali Ngemela na kuongeza

“Huu ujumbe uwafikie Wote ambao mmejipanga kubeba mabegi ya wagombea…acheni hizo tabia hazifai mtafukuzwa kazi”

Kanali Lubinga aliwasili Mkoani Geita Juni 14 Mwaka huu kwa ajili ya kufanya ziara ya siku Tatu ya kukagua Miradi mbalimbali ya Maendeleo chini ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Mahandishi Robert Gabriel.

Akiwa Wilayani Geita Kanali Lubinga alitembelea na kukagua mradi wa EPZ pamoja na Mradi wa Ujenzi wa soko la Katundu na kupanda Miti.

Pia Kanali Lubinga alitembelea mradi wa Soko Kuu la Dhahabu,sambamba na kukagua Ujenzi wa vibanda vipya vya soko Kuu la Dhahabu.

Aidha akiwa wilayani Geita Kanali Lubinga alikagua Ujenzi wa machinjio ya kisasa Mpomvu pamoja na mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Katoro.

Akiwa wilayani Mbogwe Kanali Lubinga alikagua Ujenzi wa vyumba vya madarasa, Bweni pamoja na Bwalo la Chakula katika shule ya sekondari Nyakasaluma, pamoja na Ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kasandalala.

Wilayani Chato Kanali Lubinga alikagua Ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mlimani, na Ujenzi wa Ofisi za CCM Tawi la Bomani, pamoja na kukagua Ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Chato.