Home Biashara Zaidi ya wafanyabiashara 2000 wapatiwa elimu ya kodi Ilala

Zaidi ya wafanyabiashara 2000 wapatiwa elimu ya kodi Ilala

0

Mfanyabiashara wa duka akimuonyesha Afisa wa Kodi TRA  Lameck Ndinda nyaraka mbalimbali za biashara​

Afisa Msimamizi wa Kodi TRA, Lameck Ndinda katika mojawapo ya maduka eneo la Tabata Bonyokwa

Afisa Msimamizi wa Kodi TRA, Isihaka Sharif akimuelekeza jambo mfanyabiashara.

******************************

By Oliver Njunwa

Zoezi la kuelimisha walipakodi katika maeneo ya biashara zao (mlango kwa mlango) ambalo linafanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Mkoa wa kodi Ilala limeendela kwa mafanikio ambapo jumla ya wafanyabiashara 2,165 wamepatiwa elimu katika siku sita za zoezi hilo.

Wafanyabiashara waliopatiwa elimu ni katika maeneo ya Tabata, Relini, Bima, Liwiti, Barakuda, Kimanga, Segerea, Kinyerezi, Kisiwani na Bonyokwa Mkoa wa Kodi wa Ilala.

Akizungumzia zoezi hilo Afisa Msimamizi wa Kodi TRA Ilala, Zakeo Kowelo amesema kwa ujumla zoezi limeenda vizuri kwani wafanyabiashara wametoa ushirikiano wa kutosha kwa kutoa taarifa muhimu na kuonyesha nyaraka ambazo zilihitajika jambo ambalo limewawezesha kuwapa ushauri na elimu inayostahili. “Kwa hili tunawashukuru sana kwani tumeweza kuwaelimisha kama tulivyopanga”, alisema Kowelo

Bw. Kowelo amesema zoezi lilihusisha kupita duka kwa duka na kuangalia taarifa za wafanyabiashara za kodi ambapo baada ya kuangalia taarifa walifanya majadiliano na kumshauri mfanyabiashara jinsi ya kutunza kumbukumbu. “Kwa wale ambao hawajasajili biashara zao wanaelekezwa taratibu za kusajili ili watambulike kuwa walipakodi”, alisema Kowelo.

Pamoja na kusajili biashara pia wafanyabiashara wameshauriwa jinsi ya kujisajili na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na wale wanaostahili kutumia mashine za kodi za kielektroniki wamepewa utaratibu wa kupata na kuzitumia mashine hizo.

“TRA ni sehemu ya biashara za wananchi hivyo lengo letu ni kuwaelimisha wananchi ili wafanye biashara kwa usalama zaidi na kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi sahihi na kwa wakati’, alisema Kowelo.

Aidha amewasihi wafanyabiashara kuendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo ambalo ni endelevu na muhimu kwa ukuaji wa biashara na mapato ya serikali.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara ambao wametembelewa wakati wa zoezi hilo, wameishukuru na kuipongeza TRA  kwa uamuzi wa kuwafuata katika maeneo yao ya biashara kwa kusema kwamba hayo ni mabadiliko makubwa ambayo yanaongeza uhusiano mzuri kati ya TRA na walipakodi na pia kuongeza hamasa ya kulipa kodi kwa hiyari.

“Hili ni zoezi muhimu kwani wafanyabiashara wengi bado wanahitaji elimu ya ana kwa ana’, alisema Stewart Kimbaga mfanyabiashara ya urembo Bonyokwa. Ameongeza kwamba pamoja na elimu kutolewa katika vyombo mbalimbali vya habari sio wananchi wote wanaopata taarifa hizo hivyo kutembelea walipakodi na kuwaelimisha katika maeneo yao ya biashara ni jambo la kupongezwa.

Bw, Kimbaga akasema kwamba baadhi ya wafanyabiashara hawana uelewa wa jinsi ya kufanya biashara ikiwa ni pamoja na utaratibu mzima wa kulipa kodi kwa hiyo fursa hii ni muhimu kwa wote ambao wanafanya biashara bila uelewa wa taratibu za kuanza na kufanya biashara. “Mwananchi akipata mtaji wake na sehemu ya kufanya biashara anadhani amemaliza kila kitu kwa sababu hajui anaanzia wapi wala aende wapi. Kwa hiyo akifungiwa biashara yake anaona kama anaonewa’, alisema Bw. Kimbaga na kuongeza kwamba kutokana na elimu inayotolewa sasa wananchi watafanya biashara kwa kufuata utaratibu.

Pamoja na kutoa pongezi hizo Bw. Kimbaga akasema kwamba ukaguzi peke yake hautoshi bali unatakiwa uambatane na elimu ili kuwaongezea wananchi uelewa na kujenga uhusiano mzuri baina ya TRA na walipakodi

Naye Dr. Kisinza ambaye ni mmiliki ya nyumba ya kulala wageni na kumbi za mikutano anasema kwamba kwake yeye anaona mabadiliko makubwa kwa sababu TRA imekuwa karibu sana na wafanyabiashara.

Akasema kwamba ili zoezi hili lifanikiwe zaidi ni vema liwe endelevu na lisiegemee Dar es salaam pekee bali elimu itolewa mikoa yote ili wananchi wengi waelewe taratibu zinazostahili kufuatwa, waweze kueleza wasiwasi wao na kutoa maoni.

“Hili litaongeza ridhaa ya wananchi kulipa kodi kwa hiari na hivyo kuongeza mapato ya serikali kwani hakuna taifa ambalo limeendelea bila kukusanya kodi”, alisema Dr. Kisinza.

Zoezi la kutembelea walipakodi katika maeneo yao ya biashara ni mkakati ambao TRA inautekeleza ili kuwaelimisha walipakodi, kuwapa ushauri wa kitaalamu kuhusu taratibu za kulipa kodi, kusajili biashara ambazo hazijasajiliwa, kuwakumbusha kulipa kodi, kutatua changamoto zinazo wakabili na kupata maoni yao kuhusu huduma inayotolewa na TRA kwa ajili ya kuboresha utendaji wake