Home Mchanganyiko TAKUKURU YAMFIKISHA MAHAKAMANI MWENYEKITI WA SOKO KWA KUTOA RUSHWA 

TAKUKURU YAMFIKISHA MAHAKAMANI MWENYEKITI WA SOKO KWA KUTOA RUSHWA 

0
……………………………………………………………………………..

Na.Joseph Lyimo,Manyara

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, imemfikisha kwenye Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la Mirerani, Yesaya Songelaeli Yindi kwa makosa ya rushwa. 
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkuu wa Takukuru mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu, Juni 9 mwaka huu, Songelaeli ameshtakiwa kwa kosa la kutoa rushwa ya shilingi 407,000 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Yefred Myenzi. 
Makungu alisema katika kesi hiyo namba 47/2020 Songelaeli ameshtakiwa kwa kutoa rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1) (b) na 15 (2) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007. 
Alisema katika kesi hiyo iliyopo mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya hiyo, Charles Uiso na wakili wa TAKUKURU, Adam Kilongozi, mfanyabiashara mwingine Antipas Benedict Ngelesh aliunganishwa kwenye kesi hiyo. 
Alisema uchunguzi wa TAKUKURU wilayani Simanjiro ulibaini kuwa Mkurugenzi Myenzi alitoa maelekezo ya kubomolewa kwa kibanda cha kuoshea magari cha Ngelesh kilichojengwa kinyume na utaratibu katika eneo la kitega uchumi Mirerani. 
“Songelaeli akiwa ni Mwenyekiti wa wa wafanyabiashara wa eneo hilo mwenye ushawishi mkubwa alichukua fedha hizo za rushwa na kuzituma kwa Mkurugenzi ili amshawishi abadili uamuzi wa kuvunja kibanda hicho,” alisema Makungu. 
Hata hivyo, washtakiwa hao wamekana mashtaka dhidi yao na wapo nje kwa dhamana na kesi hiyo itaendelea mahakamani hapo Julai 02 kwa usikilizaji wa awali. 
Makungu alitoa wito kwa wakurugenzi watendaji wa Halmashauri na watumishi wote wa umma wa mkoa wa Manyara na Tanzania kwa ujumla kuiga hatua zilizochukuliwa na Myenzi. 
Alisema viongozi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za wafanyabiashara wanaowashawishi kwa kuwapa rushwa ili kutotekeleza majukumu yao ya kisheria na kwa utaratibu huo rushwa itapungua kwa kiasi kikubwa ndani ya muda mfupi ndani ya Manyara na Tanzania kwa ujumla