Home Mchanganyiko TARI- Selian Yatimiza ndoto ya Tanzania ya Viwanda

TARI- Selian Yatimiza ndoto ya Tanzania ya Viwanda

0

…………………………………………………………………………….

  • Yatokomeza Utapiamlo nchini

Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

“Tafiti zetu zimelenga kutatua changamoto za wakulima hasa katika maeneo ya kuongeza tija ya uzao wa mazao yao, Kituo chetu kimegundua aina mbalimbali za mbegu zenye uzao mkubwa ili kuwasaidia wakulima kupata tija ili waweze kujiongeza kipato sambamba na kuboresha maisha yao. Aidha, eneo jingine tunaloangalia ni kuondoa changamoto inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi kama vile ukame, na hivyo tumezalisha mbegu za mahindi zinazostahimili ukame na kusambaza kwa wakulima waliopo sehemu mbalimbali hapa nchini”

Hayo yanasemwa na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo -Selian, Dkt. Joseph Ndunguru wakati akizungumza na Afisa Habari kutoka Idara ya Habari – MAELEZO na mwandishi wa makala hii, Immaculate Makilika alipotembelea kituo hicho hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Dkt. Ndunguru, Kituo hicho  kina mchango mkubwa katika kuboresha afya ya walaji, ambapo  kimegundua mbegu zenye kiwango kikubwa cha virutubisho, kama vile maharage lishe yenye kiwango kikubwa cha madini ya zinki pamoja na madini ya chuma ambayo yanasaidia kuongeza uzalishaji wa damu na  kuongeza kinga ya mwili kwa mlaji.

Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni katika kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda kama ambavyo Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ameelekeza mara kadhaa, TARI- Selian nayo imeendelea kutekeleza azma hiyo kwa kumpa mkulima ujuzi wa kuchakata mazao mbalimbali ili kuongeza thamani.

Dkt. Ndunguru anasema,“Tunataka sasa mkulima asitegemee tu kuuza mbegu tunampa teknolojia na ujuzi wa kuchakata mazao mbalimbali  ili kupata bidhaa tofauti tofauti ambazo zinaweza kuingia sokoni ili na wao waweze kutoa mchango mkubwa katika uchumi wetu wa viwanda”. 

Dkt. Ndunguru anabainisha kuwa ili kusaidia kukuza sekta adhimu ya kilimo nchini TARI- Selian imeendelea kufanya utafiti wa ubora wa udongo kwa kuangalia tabia zake na kutengeneza ramani ambazo zinaonesha taarifa mbalimbali za udongo ili kusaidia kufanya uamuzi wa aina ya zao linalofaa kulingana na aina ya udongo.

Kwa upande wake, Mtafiti wa Magonjwa ya Mimea, Edith Kadege anasema kuwa TARI-Selian imezalisha mbegu 15 kati ya aina 42 zilizozalishwa katika vituo mbalimbali hapa nchini. Aidha, kati ya aina hizo 15, kuna aina saba za mbegu zilithibitishwa mwaka 2018. Kati ya hizo, aina mbili ya mbegu zina sifa ya kukomaa mapema na kustahimili ukame, huku aina nyingine mbili za mbegu zina madini ya chuma na zinki ambayo huitwa maharage lishe.

“Kwa hali ya sasa kumekuwa na changamoto ya wanawake wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano wana upungufu wa damu, kwa hiyo aina hizi mbili ni mpango mkakati kwa wakulima ili wazalishe maharage ya kutosha na kwa vile watanzania tunakula maharage karibu kila siku na hivyo itasaidia tatizo la upungufu wa damu na utapiamlo”, anasema Bi. Kadege.

Bi. Kadege anaendelea kwa kusema kuwa kati ya aina saba za mbegu zilizothibitishwa mwaka 2018, kuna aina tatu za mbegu za maharage ambazo ni Selian 9, Selian 10 na Selian 11 zikiwa ni mpango mkakati katika kutimiza azma ya Serikali ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. 

Mbegu hizo zinaweza kusindikwa, kupakiwa kwenye makopo na kuuzwa kwenye maduka na mtumiaji anaweza kutumia moja kwa moja bila kuyapika tena na hivyo yanapunguza matumizi ya mkaa na muda.

Aidha, anabainisha kuwa, “Wakulima wanaweza kuzalisha mbegu hizi kwa wingi na kuuzwa katika  soko la ndani na nje ya nchi na hivyo itasaidia kuongeza viwanda nchini, na wakulima na wafanyabiashara wataongeza kipato na kuchangia uchumi wa nchi, na hivyo kwa sasa  hatuhitaji kununua mbegu hizi kutoka nje ya nchi, zinapatikana kwa wakulima hapa hapa nchini” 

Aidha, Mratibu Msaidizi wa Zao la Mahindi Nchini, Zabron Msangi anasema kuwa zao la mahindi nalo limekuwa na changamoto kadhaa kwa wakulima hasa changamoto ya uzaaji, na hivyo Kituo cha Utafiti za Mazao (TARI-Selian) kimegundua mbegu aina tatu za mahindi ambazo ni Selian H 115, Selian H 308  na Selian MH 07 ambazo zina uwezo wa kuzaa kwa wingi.

Bw. Msangi anasema,“Tumezalisha aina tatu za mbegu zitakazoweza kustahimili ukame ambazo ni Stuka M1, Stuka 1 na Vumilia K1 kwa hiyo tunawashauri wakulima kutumia mbegu za aina hiyo.”

Vilevile, katika shughuli zinazofanywa baada ya mavuno, Kituo cha Utafiti (TARI- Selian) kwa kushirikiana na wadau  kimevumbua mashine ya kupukuchua mazao ya nafaka na mikunde ili kusaidia wakulima na upotevu wa mazao ya shambani.

Aidha, katika kusaidia jamii kwa ujumla Kituo hicho kimeweza kusambaza maharage lishe katika shule za msingi 225 ambazo zina mpango wa kula chakula cha mchana shuleni zilizopo katika mikoa ya Manyara, Mbeya, Songwe, Kagera, Njombe, Kigoma, Mara, Singida, Arusha na Kilimanjaro ikiwa ni faida ya utafiti wao.

Mwisho