Home Mchanganyiko POLISI ARUSHA WAPONGEZWA KUPUNGUZA MATUKIO YA UHALIFU

POLISI ARUSHA WAPONGEZWA KUPUNGUZA MATUKIO YA UHALIFU

0

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Mashaka Gambo akisisitiza Jambo wakati  akiongea na Maafisa na Askari wa Polisi Kata Mkoa wa Arusha katika kikao kazi cha kukumbushana wajibu wa Polisi kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Kikao hicho kimefanyika katika Bwalo la Maafisa wa Polisi Arusha leo tarehe 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Jonathan Shanna akiongea na Maafisa na Askari wa Polisi Kata Mkoa wa Arusha katika kikao kazi cha kukumbushana wajibu wa Polisi kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Kikao hicho kimefanyika katika Bwalo la Maafisa wa Polisi Arusha leo

Wakuu wa Polisi toka Wilaya zote Saba za  Mkoa wa Arusha wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo wakati akizungumza na Maafisa na Askari Kata katika kikao kazi cha kukumbushana wajibu wa Polisi kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Kikao hicho kimefanyika katika Bwalo la Maafisa wa Polisi Arusha


Waratibu Tarafa na Askari Kata 157 toka kata zote za Mkoa wa Arusha walioshiriki katika kikao kazi cha kukumbushana wajibu wa Polisi kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Kikao hicho kimefanyika katika Bwalo la Maafisa wa Polisi Arusha leo 

…………………………………………………………………

Na Gasto Kwirini wa Jeshi la Polisi Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kufanikiwa kupunguza na kudhibiti matukio ya uhalifu hali ambayo imepelekea shughuli za kiuchumi kufanyika kwa amani hasa utalii.

Alitoa pongezi hizo wakati akifungua kikao kazi kilichohusisha Maafisa wa Polisi pamoja na Polisi Kata 157 toka kata zote za Mkoa wa Arusha ambacho kilikua na lengo la kukumbushana wajibu wa Polisi Kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Amesema kuwa kupitia Jeshi la Polisi, Mkoa wa Arusha kwa sasa matukio makubwa ya uhalifu yamepungua kwa kiasi kikubwa huku akitolea mfano mauaji na kubakwa kwa wanawake katika kata ya Olasiti ambapo kwa sasa matukio hayo yamedhibitiwa.

‘‘Jana nimefanya ziara katika kata Olasiti, kata ambayo ilikuwa inasumbua sana kwa mauaji ya akina Mama, jana wametoa pongezi wakasema sasa tunalala, akina mama wanatembea masaa 24 kifua mbele kwa sababu ya uwepo wa Jeshi la Polisi’’. Alisema  Gambo

Aidha aliwataka Maofisa pamoja na Askari hao kuhakikisha  uchaguzi Mkuu ujao  unafanyika  kwa amani na utulivu. Pia alisisitiza mapambano dhidi ya uhalifu na wahalifu yaendelee ili Mkoa uendelee kuwa shwari wakati wote.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shanna alisema kuwa  Jeshi la Polisi  mkoani hapa litaendelea kufanya kazi kwa weledi na nidhamu kuhakikisha matukio yote ya kihalifu yanadhibitiwa.

Aliongeza kwa kusema watahakikisha uchaguzi ujao unafanyika kwa amani na utulivu bila kutumia nguvu kubwa hasa mabomu ya machozi na silaha za moto badala yake litahakikisha linalinda amani kwa raia.

Aliwataka Wanasiasa na Wananchi kufanya siasa za kistaarabu, na kwa wale wachache ambao hupenda kuvuruga amani wakati wa uchaguzi kuacha fikra hizo kwani watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Katika Kikao hicho Askari hao walipata fursa ya kufundishwa mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ugunduzi na Upelelezi wa Makosa ya Uchaguzi, ushirikishwaji wa jamii katika kufanikisha uchaguzi, elimu  juu ya haki za raia katika uchaguzi na utayari wa Jeshi la Polisi katika kipindi chote kabla, wakati na baada ya uchaguzi.