Home Mchanganyiko MAMBA CEMENT YATUMIA MIL.500 KUTENGENEZA MATENKI 2,000 YA KUHIFADHIA MAJI ILI KUPAMBANA...

MAMBA CEMENT YATUMIA MIL.500 KUTENGENEZA MATENKI 2,000 YA KUHIFADHIA MAJI ILI KUPAMBANA NA CORONA

0

*****************************

NA MWAMVUA MWINYI
KAMPUNI ya Mamba Cement chini ya Kampuni Mama ya MM Steel, imetumia kiasi cha sh.milioni 500 kutengeneza Matenki 2,000 ya kuhifadhia maji ikiwa ni mkakati wa kupambana na ugonjwa wa Corona.
Matenki hayo yaliyosambazwa nchi nzima kwa maana ya Tanzania Bara na upande wa Visiwani, Bara yamepatiwa matenki 1000 katika taasisi za Serikali, taasisi binafsi 500 wakati Tanzania Visiwani wakinufaika na matenki 500.
Hayo yalibainishwa na Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Aboubakary Mlawa, akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kumkabidhi Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Zainab Kawawa, matenki 17 kwa ajili ya shule za Sekondari na Vyuo wilayani hapa.
Alisema ,baada ya janga la ugonjwa huo waliwasiliana na Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, ili Kampuni iweze kuyatengeneza matenki hayo kisha kusambaza katika maeneo hayo, zikiwemo na ndoo za maji tiririka, mabeseni pamoja na sabuni.
“Kampuni yetu imekuwa wadau wakibwa wa Serikali katika kusaidia nyanja mbalimbali, mara kadhaa tumekuwa mstari wa mbele kusaida katika majanga na miradi ya kimaendeleo nasi pasipo ajizi tunaungana katika masuala husika,” alisema Mlawa.
Akizungumza baada kupokea matenki hayo, Kawawa alishukuru Kampuni hiyo kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata kutokea kwenye ofisi hizo, ambapo imekuwa na msaada mkubwa katika shughuli tofauti za kimaendeleo.
Aliongeza kwamba baada ya kuwepo kwa ugonjwa huo wa Corona, walimwandikia barua Mkurugenzi Patel wakimuomba msaada wa matenki hayo yatayosambazwa kwenye shule na vyuo, malengo makubwa yakiwa kupambana na ugonjwa huo.
Akishukuru kwa niaba ya walimu wa shule za sekondari kidato cha tano na sita pamoja na vyuo, Mwalimu Victoria Kesi Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Uktubi na Uhifadhi wa nyaraka alianza kuishukuru ofisi ya Mkuu wa wilaya kwa juhudi zake, sanjali na uongozi wa Mamba Cementi kwa msaada huo.