Home Mchanganyiko SIMANJIRO YATOA MIKOPO YA SHILINGI MILIONI 244.6

SIMANJIRO YATOA MIKOPO YA SHILINGI MILIONI 244.6

0

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Yefred Myenzi akizungumza wakati wa utoaji wa mikopo ya sh244.6 milioni kwa vikundi 51 vya wanawake, vijana 20 na wenye ulemavu watano jana.

******************************

HALMASHAURI ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imetoa mikopo ya shilingi milioni 244.6 Kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye walemavu wa kata 18 kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Yefred Myenzi akizungumza wakati wa utoaji wa mikopo hiyo isiyo na riba alisema wanachama 1,412 wakiwemo wanawake 1,075 vijana 332 na wenye ulemavu watano wamenufaika na mikopo hiyo.

Myenzi alisema wanufaika wa mikopo hiyo ni vikundi 51 vya wanawake waliopatiwa shilingi milioni 171.6, vijana 20 waliopatiwa shilingi milioni 68 na kikundi kimoja cha watu watano wenye ulemavu shilingi milioni 5.

Aliwashukuru madiwani na wataalamu wa halmashauri hiyo kwa ushirikiano waliompa kwani wamefanikiwa kutoa mikopo kwa asilimia 100 ya ile asilimia 10 ya mapato yao ya ndani.

“Sasa hivi hatuna deni tena na tumepiga hatua kubwa Simanjiro kutoka shilingi milioni 5 ya mikopo iliyokuwa inatolewa mwaka 2014/2015 sasa hivi 2019/2020 inatolewa shilingi milioni 244.5 na zaidi,” alisema Myenzi.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula akizungumza wakati akikabidhi hundi kwa vikundi hivyo amewataka vijana kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo isiyo na riba.

Mhandisi Chaula alisema serikali ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli imepitisha utoaji wa mikopo kuwa lazima na siyo hiyari kwa lengo la kunyanyua sekta hizo zisizopatiwa mikopo kwenye taasisi za fedha kwa kukosa mitaji.

Ofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Asia Ngalisoni alisema kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020 jumla ya shilingi milioni 101.7 zilizokopwa zimerejeshwa.

Ngalisoni alisema kuna baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo idadi ndogo ya vikundi vya watu wenye ulemavu na vikundi vya vijana kukosa sifa ya kukomesha kutokana na kigezo cha umri.

Alitaja changamoto nyingine ni umbali wa vijiji na makao makuu ya wilaya inayosababisha gharama ya usafiri na malazi wakati wa kufuatilia mikopo kwa vikundi na kufanya marejesho.

Mmoja kati ya wanufaika wa mikopo hiyo Halima Abdalah wa kikundi cha Kipaji cha mji mdogo wa Mirerani alisema kupitia mkopo wa shilingi milioni 5 walioupata wataweza kujinyanyua kiuchumi wao binafsi na kurejesha mkopo wao.

Mmoja kati ya wana kikundi cha nguvu ya kijana wa Orkesumet, Nasoro Bakari alishukuru kwa kutolewa kwa mikopo hiyo kwani vijana badala ya kufanya vitendo vya uhalifu wanajiajiri na kufanya kazi.

Mwana kikundi wa Lukundane wa kata ya Langai, Mary Milao alisema wanawake wa eneo hilo wana mwamko mkubwa wa kufanya kazi kupitia mikopo hiyo iliyotolewa na halmashauri ya wilaya hiyo.