Home Michezo MCHEZAJI NA KATIBU MKUU WA ZAMANI YANGA AFARIKI DUNIA

MCHEZAJI NA KATIBU MKUU WA ZAMANI YANGA AFARIKI DUNIA

0

BEKI wa zamani wa klabu ya Yanga, Lawrcence Mwalusako amefariki dunia alfajiri ya leo katika hospitali ya Muhimbli alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
Kwa mujibu wa mjomba wa marehemu, Augustino Mwakyembe – Mwalusako ambaye pia alichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars miaka ya 1980 alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya Kiharusi. 
Msiba wa Mwalusako aliyewahi pia kuwa Katibu wa Yanga SC kwa awamu tofauti upo nyumbani kwake, Kimara Jijini Dar es Salaam na taarifa zaidi zinatarajiwa kutolewa na familia ya marehemu.

Mwalusako alijiunga na Yanga SC mwaka 1985 akitokea Pan Africans iliyomuibua akiwa bado mwanafunzo wa sekondari.
Akiwa Yanga SC, Mwalusako aliyekuwa anacheza nafasi zote za ulinzi pembeni kulia na kushoto pamoja na katikati, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na akacheza hadi mwaka 1990 alipoamua kustaafu.
Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Lawrence Mwalusako.