Home Mchanganyiko OLE SENDEKA AWATAKA WATANZANIA KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI

OLE SENDEKA AWATAKA WATANZANIA KUMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI

0
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, (kulia) akishuhudia mazishi ya mdogo wake Sumleck Ole Sendeka ambaye alikuwa Katibu mwenezi wa CCM Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, yaliyofanyika nyumbani kwao Losokonoi Kata ya Naberera.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka (kulia) akipokea rambirambi kutoka kwa Katibu wa CCM Mkoani Manyara, Naomi Kapambala kwenye msiba wa mdogo wake Sumleck Ole Sendeka ambaye alikuwa Katibu mwenezi wa CCM wilayani Simanjiro aliyezikwa nyumbani kwao Losokonoi Kata ya Naberera.
Linna Sendeka akisoma wasifu wa aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM Wilayani Simajiro Mkoani Manyara,marehemu Sumleck Ole Sendeka aliyezikwa nyumbani kwao Losokonoi Kata ya Naberera.
…………………………………………………………………………………………
WATANZANIA wametakiwa kuwa kitu kimoja na kumuunga mkono Rais John Magufuli kwenye kipindi hiki cha mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona kwani ameonyesha msimamo ambao hivi sasa unaigwa na baadhi ya nchi mbalimbali duniani. 
Mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka aliyasema hayo nyumbani kwao Losokonoi mkoani Manyara, akizungumza kwenye maziko ya katibu mwenezi wa CCM wilayani Simanjiro, Sumleck Ole Sendeka ambaye ni mdogo wake. 
Ole Sendeka alisema anawaomba watanzania wamuunge mkono Rais Magufuli kwa namna alivyosimama kidete kwenye mapambano ya corona kwani ameonyesha msimamo mkubwa kutokana na uongozi wake mahiri, thabiti wenye msimamo usiyoyumbishwa. 
Alisema hatua zilizochukuliwa na Rais Magufuli kwenye vita ya corona hivi sasa zimeigwa na baadhi ya nchi, japo baadhi ya nchi jirani zilitumiwa na mabeberu kuchafua taswira nzuri ya Tanzania kwa kutumiwa na mabeberu. 
“Serikali ya awamu ya tano haitayumba wala kutikisika kiuchumi kwani Mungu ametupa rasilimali mbalimbali hivyo tumuunge mkono Rais Magufuli na nawahakikisha tutazidi kusonga mbele,” alisema Ole Sendeka. 
Alisema kupitia msiba huo ameshuhudia wananchi wa vijiji vyote vya wilaya hiyo kufika nyumbani kwao Losokonoi kata ya Naberera kwa ajili ya kumsindikiza marehemu Sumleck. 
“Pamoja na hayo nawashukuru wote walishiriki ikiwemo kamati ya mazishi iliyoongozwa na Mathias Manga na Monabani aliyenunua barakoa 1,000 kwa ajili ya watu kuvaa hapa mazikoni,” alisema. 
Mbunge wa jimbo la Simanjiro, James Ole Millya alimpongeza Rais Magufuli kwa kuruhusu shughuli za maziko kufanyika kwani awali ilikuwa mtu akazikwa na watu 10 kwa hofu ya corona. 
Ole Millya alisema marehemu Sumleck amepata heshima kubwa ya kuzikwa na wana Simanjiro wenzake hasa wana CCM ambao walitaka kushuhudia safari yake ya mwisho. 
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula aliwataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kuchukua tahadhari ili wasipate maambukizi mapya ya corona kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya. 
Chaula alisema marehemu Sumleck alikuwa kijana mahiri na msikivu ambaye alikuwa atashirikiana na serikali ya wilaya hiyo kwenye mambo mbalimbali. 
Linna Ole Sendeka akisoma wasifu wa marehemu Sumleck alisema alizaliwa mwaka 1968 akiwa mtoto wa saba wa marehemu mzee Olonyokie na kufariki Mei 16 mwaka 2020.
Alisema wakati wa uhai wake marehemu Sumleck aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo diwani wa kata ya Naberera, mwenezi wa CCM wilaya ya Simanjiro na mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa. 
Alisema marehemu alikuwa anasumbuliwa na tatizo la kifua, lililomsumbua kwa nyakati tofauti na kutibiwa hospitali mbalimbali za wilayani Simanjiro na jijini Arusha.