Sheikh wa mkoa wa Mwanza Alhaji Hasani Kabeke (kushoto) akizungumza na waandishi w habari kuhusu dua ya siku tatu ya kumwomba na kumshukuru Mungu kwa kusikia maombi ya Watanzania kuwaepusha na mambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.
………………………………………………………………………………….
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BWAKWATA) Mkoa wa Mwanza, limesema waumini wa dini hiyo mkoani humu wataungana na wa mikoa mingine nchini kufanya ibada ya kuomba dua kumshukuru Mungu kwa kusikia na kujibu maombi ya Watanzania kuhusiana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19).
Pia watafanya ibada ya kumwombea dua Rais John Magufuli, Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda kwa alichokionyesha na hatua alizochukua za kuwapigania wananchi wanyonge kwenye mapambano ya ugonjwa wa corona ili kuwaepusha na maambukizi ya ugonjwa huo.
Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke akizungumza na waandishi wa habari jana alisema Baraza la Ulamaa limetenga siku tatu za kufanya dua ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, itakayofanyika kuanzia leo Mei 22 hadi 24, mwaka huu.
Alisema licha ya kuwepo kwa ugonjwa wa Covid-19 mkesha wa ibada ya Ramadhani (usiku wenye cheo) mkesha huo umeruhusiwa na utafanyika kwa kufuata nidhamu ya afya kwa waumini kuzingatia uvaaji wa barakoa, kutawaza nyumbani na kwenda na miswala yao pamoja na kunawa mikono kwa mjitiririka.
Sheikhe huyo wa mkoa alisema siku hiyo ya Mei 28 au 29, hakutakuwa na chakula cha pamoja badala yake waumini wa dini hiyo waendee na chakula chao (daku) na wazee wenye umri wa miaka 65 na wenye maradhi kama kisukari wabaki na kuswali nyumbani badala ya msikitini.
“Swala Idd haitaswaliwa kwa pamoja kama ilivyozoeleka, lengo ni kuwalinda na kuwasaidia watu wetu kujikinga na maambukizi ya Corona, swala hiyo itaswaliwa kila msikiti kwa kuzingatia maelekezo.Pia itasomwa dua maalumu ya Waislamu (Khumti) siku ya swala ya Idd kwa sababu Mwenyezi Mungu amejibu maombi yao na ya Watanzania kwenye kipindi hiki cha janga la Corona,”alisema Sheikhe Kabeke.
Aidha, Baraza la Idd halitakuwepo, hivyo viongozi na waumini wa ngazi ya vijiji, kata na wilaya wajizuie kufanya mabaraza hayo na kuwasistiza kusoma mara 100 dua maalumu ya shukrani “Allah huma lakalihamundu kamaa yaanibaghi Lijalal hajihika waadhin sun twaanika (Ee Mwenyezi Mungu wewe ndiye mwenye sifa kama inavyotakikana katika utukufu na dhati yako na ukubwa wa Ufalme wako).”