Home Mchanganyiko PROF.NDALICHAKO ATANGAZA RASMI SIKU YA MITIHANI KIDATO CHA SITA

PROF.NDALICHAKO ATANGAZA RASMI SIKU YA MITIHANI KIDATO CHA SITA

0

……………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako amesema mitihani ya kidato cha sita  itaanza rasmi Juni 29 hadi 16 huku pia akiwataka wanafunzi wa kidato cha sita wale wa shule za bodi kuanza kuripoti shuleni mei 30 mwaka huu.

Kauli hii ameitoa leo  jijini Dodoma wakati akizingumza na waandishi wabari, Ndalichako amezitaka shule zote zenye wanafunzi wa kidato cha sita kufanya maandalizi ili masomo yaanze Juni Mosi,mwaka huu kama alivyotangaza Rais John Magufuli.

“Wanafunzi watakapofungua shule waendelee na masomo kama kawaida na Juni 29, mwaka huu wataanza mitihani na watamaliza Julai 16, mwaka huu,”amesema Prof.Ndalichako.

Aidha ameliagiza  Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kusambaza mitihani hiyo mara moja, lakini pia kuhakikikisha matokeo yanatoka kabla ya Agosti 30, mwaka huu ili wanafunzi watakaofanya vizuri wapate muda wa kutuma maombi vyuo vikuu bila kuathiriwa na muda.

Hata hivyo amesema kuwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Vyuo Vikuu ipo tayari na pia bodi hiyo ina fedha kiasi cha sh.bilioni 122.8 kwa ajili ya wanafunzi wenye sifa ya kupata mikopo.

Amesema, kinachotakiwa ni vyuo kuwasilisha nyaraka muhimu huku akisema hadi Mei 28, mwaka huu nyaraka hizo ziwe zimewasilishwa Bodi ya Mikopo ili itoe fedha hizo mara tu wanafunzi wanapofika vyuoni. “Mara nyingi ucheleweshaji huwa unatokea vyuoni ,tunaomba nyaraka ziwahi maana fedha zipo,”amesisitiza 

Prof.Ndalichako amevitaka vyuo vijipange na kuweka maafisa wa kutosha kufanya malipo ili kukimbizana na muda. Pia amewataka wanafunzi nao kuwasilisha nyaraka zao muhimu ili wapatiwe fedha.

Kwa upande mwingine amevikumbusha  vyuo pamoja na shule  kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona kwa kuweka ndoo za maji na sabuni katika maeneo mbalimbali .

Waziri Ndalichako ametoa wito kwa walimu pamoja na wanafunzi kuhakikisha wanajituma katika masomo yao ili waweze kukamilisha mihtasari kwa wakati bila kuathiri mwaka wa masomo 2020/2021