Home Mchanganyiko TARURA SIMIYU KUFUNGUA BARABARA ZILIZOATHIRIWA NA MVUA KUZIFANYA ZIPITIKE WAKATI WOTE

TARURA SIMIYU KUFUNGUA BARABARA ZILIZOATHIRIWA NA MVUA KUZIFANYA ZIPITIKE WAKATI WOTE

0

Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Simiyu, Eng. Dkt. Philemon Msomba akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja linalojengwa kwa mpango wa dharura katika eneo la Mto  Ndoba linalounganisha Mtaa wa Bunamhala na Majahida katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mei 13, 2020.

Ujenzi wa daraja katika eneo la Mto  Ndoba linalounganisha Mtaa wa Bunamhala na Majahida ukiendelea ambapo unatarajiwa kukamilika Mei 15, 2020 kupitia fedha za mpango wa dharura.

Ujenzi wa daraja katika eneo la Mto  Ndoba linalounganisha Mtaa wa Bunamhala na Majahida katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi ukiendelea ambao unatarajia kukamilika Mei 15, 2020 kupitia fedha za mpango wa dharura.

Ujenzi wa daraja la Mto Nyambuli linalounganisha kijiji cha Mwamondi na Lulai katika kata ya Dutwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ukiendelea ambao ambao unatarajia kukamilika Mei 15, 2020 kupitia fedha za mpango wa dharura.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) Mei 13, 2020 mjini Bariadi  juu ya kazi mbalimbali zilizofanywa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Simiyu.

Diwani wa Kata ya Dutwa, Mhe.Mapolu Mkingwa akizungumza akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati wa zaira ya Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Simiyu, Eng. Dkt. Philemon Msomba aliyoifanya Mei 13, 2020.

Lazaro Samwel mkazi wa Mtaa wa Bunamhala katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi akizungumzia ujenzi wa daraja katika eneo la Mto  Ndoba linalounganisha Mtaa wa Bunamhala na Majahida ukiendelea ambao unatarajia kukamilika Mei 15, 2020.

Magreth Magile mkazi wa Mtaa wa Bunamhala katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi akizungumzia ujenzi wa daraja katika eneo la Mto  Ndoba linalounganisha Mtaa wa Bunamhala na Majahida ukiendelea ambao unatarajia kukamilika Mei 15, 2020.

…………………………………………………………………………………..

Na Stella Kalinga, Simiyu

Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Simiyu, Eng. Dkt. Philemon Msomba amesema Serikali imedhamiria kufungua barabara zote zilizoharibiwa na mvua mkoani hapa na kuhakikisha zinapitika kwa mwaka mzima ili kuwarahisisha wananchi  mawasiliano na usafirishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali.

Dkt. Msomba ameyasema hayo Mei 13, 2020 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa madaraja katika wilaya ya Bariadi eneo la Mto  Ndoba linalounganisha Mtaa wa Bunamhala na Majahida litakalogharimu shilingi milioni 33 na daraja la Mto Nyambuli linalounganisha kijiji cha Mwamondi na Lulai (Dutwa) litakalogharimu kiasi cha shilingi milioni 25 yanayojengwa kwa mpango wa dharura.

“Azma ya Serikali ni kuhakikisha barabara zote zinapitika kwa mwaka mzima, tunaishukuru Serikali imetoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara mkoani Simiyu, mwaka wa fedha 2019/2020 tulitenga bajeti ya shilingi bilioni tano, kufikia Mei 13, 2020 tumepokea shilingi bilioni 4.23 sawa na asilimia 84; kwa hiyo barabara zote zilizoathiriwa na mvua tuna uhakika wa kuzifungua,” alisema Mratibu wa TARURA Simiyu, Eng. Dkt. Philemon Msomba.

Aidha, Dkt. Msomba amesema TARURA itafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa miradi yote  ikiwemo ya dharara inatekelezwa kwa kiwango na kwa wakati ili barabara hizo ziweze kuwanufaisha wananchi kiuchumi ambapo amebainisha kuwa TARURA Simiyu imeomba kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kwa mpango wa dharura.

Dkt. Msomba amesema pamoja na ujenzi wa madaraja katika mwaka wa fedha 2019/2020  TARURA imejipanga kutengeneza mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 690 huku akiwataka Mameneja wa TARURA wa wilaya kusimamia ubora wa kazi katika ujenzi huo na kuhakikisha kazi zote zinakamilika kwa wakati.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewashukuru viongozi wa TARURA kwa namna walivyochukua hatua madhubuti kuhakikisha madaraja yanatengenezwa na barabara za vijijini zinapitika hususani kwenye kipindi cha mvua nyingi, huku akitoa rai kwa viongozi hao kuwasimamia wakandarasi ili wafanye kazi kwa kuzingatia viwango vya kitaalam na thamani ya fedha.

Naye Diwani wa Kata ya Dutwa, Mhe.Mapolu Mkingwa amesema matengenezo ya daraja la Mto Nyambuli linalounganisha kijiji cha Mwamondi na Lulai utaondoa adha iliyokuwa ikiwapata wananchi kufika makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Dutwa na kurahisisha usafirishaji wa mazao kwa kuwa Mwamondi ndiyo ghala la chakula kwa kata hiyo.

Wakizungumzia ujenzi wa madaraja yaliyokuwa yamesombwa na maji kutokana na mvua wananchi wa Mtaa wa Bunamhala na Majahida katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Kulwa Nyanza, Lazaro Samwel na Magreth Magile wamesema baada ya daraja kukatika iliwalazimu kutumia usafiri wa pikipiki na baiskeli  kutokana na eneo la mto Ndoba kutopitika kwa magari.

“Tulikuwa tunapata shida kuvuka mto huu na mvua zinaponyesha tulikuwa tunalazimika kutengeneza daraja la miti ili litusaidie kuvuka, tunaishukuru serikali kuchukua hatua za kuanza kujenga daraja tunaomba likamilike mapema maana huku kuna wananchi wengi na vile vile kuna chuo cha maendeleo ya jamii,” alisema Lazaro Samwel.

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Simiyu unahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 4038.16 ambapo kati ya hizo asilimia 55 zinapitika na ziko katika hali nzuri na wastani, huku asilimia 45 ya mtandao zinahitaji matengenezo na jitihada zinafanyika ili zifanyiwe matengenezo kuhakikisha zinapitika kwa mwaka mzima.