Home Mchanganyiko WAMILIKI WA VIWANDA WATAKIWA KUZALISHA VIFAA KINGA KUKABILIANA NA CORONA

WAMILIKI WA VIWANDA WATAKIWA KUZALISHA VIFAA KINGA KUKABILIANA NA CORONA

0

Waziri Ummy Mwalimu na Waziri Innocent Bashungwa wakiwa kwenye kikao na Umoja wa wazalishaji wa Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba wakati wa mkutano huo

Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiongea na Umoja wa Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini wakati wa kikao cha kujadili namna ya uzalishaji wa vifaa kinga vya kukabiliana na Corona nchini

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Brig.Gen Gabriel Saul Mhidze(Dkt) akiongea wakati wa kikao hicho

Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa akiongea wakati wa kikao hicho ambapo amewapongeza wamiliki wa viwanda vya dawa,vifaa na vifaa tiba kuzalisha vifaa kinga .

Waziri Ummy Mwalimu akiangalia ngao ya uso( Face Shield) ambayo inazalishwa na viwanda hapa nchini

Wazalishaji wa dawa,vifaa na vifaa tiba wakionesha nguo ya kujikinga ambayo itaanza kutengeneza na baadhi ya viwanda nchini

****************************

Na.WAMJW- Dar es Salaam

Wamiliki wa viwanda vya Dawa, Vifaa na vifaa tiba nchini wametakiwa kuanza kuzalisha vifaa kinga kuweza kukabiliana na janga la Corona nchini ili kuondokana na changamoto ya ucheleweshaji wa kupata vifaa kinga toka nje ya nchi pamoja na kupunguza gharama.

Wito huo umetolewa leo jijini hapa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akiongea na Umoja wa Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini kwenye mkutano wa kuangalia jinsi gani wanaweza kuzalisha vifaa kinga kutoka wazalishaji wa ndani hapa nchini.

“Tukizalisha hapa nchini tutaokoa rasiliamali fedha nyingi, muda pia tutazalisha ajira na kuwa na uhakika wa ubora na usalama unaohitajika kupitia mamlaka zetu za ndani kwa urahisi”. Alisema Waziri Ummy.

Waziri amesema kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa vifaa kinga , hivyo wale wote wanaozalisha vifaa kinga wanatakiwa kuongeza uzalishaji ili kutosheleza mahitaji ya soko nchini na hata kuweza kuuza nchi za jirani.

Aidha, amesema Wizara inahitaji kuipa nguvu huduma salama kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali na visivyo vya Serikali kwa watumishi wa afya kuzingatia miongozo ya kukinga na kudhibiti maambukizi angalau kuvaa barakoa,glove na eproni hivyo amewasisitiza kuzalishaji vifaa vyenye viwango vyenye ubora ili kukidhi soko la ndani nan chi za jirani.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa amewapongeza wamiliki wa viwanda hivyo kwa kubuni na kugundua teknolojia na uzalishaji wa vifaa kinga kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.

“Kuanzisha viwanda ni sehemu ya ulinzi wa nchi,hivyo kuwa na viwanda vyetu nchini hususani wakati wa shida imesaidia upatikanaji wa baadhi za vifaa kinga kwa bei nafuu”.Alisema Waziri Bashungwa
Amesema katika kikao hicho wamekubalia kujipanga vizuri katika uzalishaji wa vifaa kinga na hivyo wamewataka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kujikita katika kuzalisha barakoa aina ya N95 na glove kutokana na kwamba viwanda vya namna hii havipo nchini.

Pia Waziri Bashungwa ameitaka TMDA kushirikia na wizara ya viwanda kuisaidia NDC kuweza kufanya kiwanda hicho kuanza kuzalisha kwa wakati na hivyo kusaidia watumishi wa afya walio mstari wa mbele kutoa huduma bila hofu.

Kwa upande wa MSD, Waziri Bashungwa ameitaka kununua vifaa kinga vinavyozalishwa na viwanda vya ndani ambavyo vimekidhi viwango na vimesajiliwa na TMDA badala ya kutumia fedha iliyotengwa na Serikali kununua vifaa hivyo nje ya nchi.

Waziri Bashungwa ameahidi kukitembelea kiwanda cha Msagala Investment kilichopo Bagamoyo ambacho kinatarajia kuanza kuzalisha malighafi za utengenezaji wa barakoa kutokana na pamba zinazolimwa nchini.