Home Makala MCHANGO WANGU KUHUSU MJADALA WA IDADI YA WACHEZAJI WA KIGENI

MCHANGO WANGU KUHUSU MJADALA WA IDADI YA WACHEZAJI WA KIGENI

0

…………………………………………………………………………………………..

Imani Mbaga,Madau

Kwanza kabisa nimshukuru mhe, waziri mwenye dhamana ya michezo, Dr Mwakyembe, kwa kuurasmisha huu mjadala, kwakuwa umekuwapo kwa muda mrefu katika majukwaa yasiyo rasmi.
Ni suala linalojirudia rudia, ama bungeni, kwenye “vijiwe” vyetu vya kunywea kahawa au maeneo mengine yanayohusisha wadau wa soka na mijadala yao.
Kuwa na mjadala was kitaifa no jambo lenye afya kwa michezo hasa mchezo wa mpira wa miguu ambako ndiko kuliko athirika zaidi na ujio wa wachezaji wa kigeni.
Naamini maoni ya wadau yatachangia pakubwa katika kutengeneza mfumo utakao sababisha kupunguza kama siyo kumaliza kabisa tatizo la “uholela” uliopo sasa katika suala la usajili unaogusa wachezaji wa kigeni.

Kwangu mimi naamini tatizo tulilonalo siyo idadi bali ni viwango vya wachezaji wa kigeni.
Leo hii, mjadala wa idadi ya wachezaji wa kigeni, umeibuliwa na swali la msingi, endapo wachezaji hao wana msaada wowote katika maendeleo ya soka letu. Kuhoji huko kumetokana na viwango vibovu kama siyo vya kawaida viliivyoonyeshwa na wachezaji wa kigeni tuliowashuhudia kwa takribani muongo mmoja hivi.
Kwa hiyo unaweza kuona kwamba tatizo kubwa wanalohoji wadau, siyo idadi bali ni viwango vyao, na hasa kwa kuzingatia thamani ya pesa inayotumika “value for money”.
Kabla sijatoa mtazamo wangu kuhusiana na idadi, nizungumzie kidogo matatizo makubwa matatu yaliyotufikisha hapa hadi leo tunajadiliana suala hili.
Tatizo la kwanza ni MFUMO WA KIMUUNDO wa uendeshaji wa soka la vilabu vyetu hapa nchini.
Kimsingi viwango vibovu vinavyoonyeshwa na wachezaji wa kigeni, vinatokana na mfumo mbaya wa usajili katika vilabu vyetu. Watu wengi wanaojihusisha na usajili ni watu waliopata nafasi hiyo kupitia mlango wa “ulegevu” wa mfumo wa uendeshaji wa vilabu vyetu. Hawa ni watu walio kati ya mtu anayetoa fedha za usajili na mtu atakayewatumia wachezaji husika, hawa huishi hapo kati, na lengo lao kubwa ni kujipatia fedha kupitia kile kinachoitwa asilimia 10, yaani kiwango cha juu kinachoongezwa kwenye fedha halisi ya usajili wa mchezaji. Uwepo wa watu hawa, usipodhibitiwa tutaendelea kuona kiwango kibovu cha wachezaji wa kigeni hata tukishusha idadi yao kufikia watatu tu. Namna pekee ya kumaliza tatizo la watu hawa ni kubadilisha mfumo na muundo wa uendeshaji wa vilabu vyetu.
Tatizo la pili linalotukabili ni ULEGEVU WA UTEKELEZAJI WA KANUNI ZETU, hili ni tatizo linalokabili vyama vyetu vya michezo hapa nchini. Kwa mfano, ili kupata viwango bora vya wachezaji watakaotufaa, basi ni lazima tuwe na vigezo tutakavyojiwekea jinsi na sifa ya kuwapata wachezaji wenye ubora unaofaa na wenye msaada kwa soka na taifa letu.
Katika hili ni vizuri tuwe makini, kwakuwa hakuna taifa lisilo na vigezo katika kucheza soka kwenye nchi yao. Vigezo kama viwango vya soka vya nchi anayotoka mchezaji, historia ya uchezaji wake, kwa maana ya alikopita hadi kufikia hapa, ligi alizocheza nk. Hii itatusaidia kudhibiti viwango vya wachezaji wanaoingia nchini kwetu, lakini tatizo kubwa tulilo nalo ni kwamba, ufuatiliaji wa kanuni tunazojiwekea ni suala linaloleta shida mno. Tumekuwa na udhaifu mkubwa katika kusimamia kanuni tunazojiwekea katika mambo mengi hususani kwenye soka. Hata tukipunguza idadi bado tutapata shida ya viwango ambacho ndicho kitu cha muhimu kuliko idadi kwa sasa.
Tatizo la tatu ni UCHUMI WA VILABU VYETU, hili linaweza kuwa na mjadala wa kipekee, kwa sababu bila misuli ya kiuchumi tatizo la kusajili, si wachezaji wa kigeni tu, bali hata wachezaji wa ndani litaendelea kuwa shida. Ni vema sasa mikakati ya kujiimarisha kiuchumi na kujiendesha iwe sehemu ya kanuni zinazoangaliwa kila mwanzo wa msimu ili kujiridhisha juu ya uwezo wa klabu husika. Hadi sasa kimtazamo hatuna klabu inayojiendesha lakini mbaya zaidi hatuna mikakati wala mipango ya kututoa tulipo.
Kwa kuzingatia hayo mjadala huu kwangu, unanilazimisha kuliangalia suala hili, kutoka kwenye idadi hadi kwenye ubora.

USHAURI WANGU
Ninachoshauri ni kuangalia mifumo yetu na kuhakikisha tunatengeneza kanuni zinazozingatia vigezo rasmi vya wachezaji kutoka nje.
Kudhani kwamba kupunguza idadi kutasaidia wachezaji wetu kukua, kupata nafasi au kujionyesha, bado halitakuwa jawabu la kufanya hayo yote, kitakachotokea ni wachezaji wetu kuridhika na “kubweteka” hali ambayo itashusha ushindani na utendaji kwa jumla.
Sishauri kupunguza idadi ya Sasa, bali tukubaliane vigezo vya wachezaji tunaowahitaji, tusimamie utekelezaji wa hilo kwa nguvu na kuhakikisha hakuna anaetumia ujanja ujanja katika utekelezaji wake.

Soka letu linategemea maamuzi bora ya namna ya uendeshaji wake, sera madhubuti na utashi wa viongozi wetu kulikuza soka.