Home Mchanganyiko WAPONGEZA UJENZI WA HOSPITALI YA MPIMBWE

WAPONGEZA UJENZI WA HOSPITALI YA MPIMBWE

0

Mkuu wa wilaya ya Mlele mkoani Katavi  yenye Halmashauri mbili ya Mlele na Mpimbwe Rechal Kassanda akielezeaa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe ambayo iko katika hatua ya mwisho kukamilika.

Picha na Mpiga Picha Maalum

…………………………………………………………………………….

Na Mwandishi Wetu,Mpimbwe

SERIKALI imepongezwa kwa mpango wake wa kujenga vituo vya Afya kila kata,ujenzi wa Hospitali za wilaya na Rufaa hatua inayotajwa imesaidia  kuboresha huduma za Afya na kuwepo kwa mazingira  ya utoaji huduma bora kwa watumishi wa sekta ya Afya katika mkoa wa Katavi.

Hayo yamesemwa kwa nyakati tofauti na baadhi ya wananchi waliokutwa wakipata matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Walisema,tangu Serikali ilipoanza  ukarabati wa zahanati na ujenzi wa vituo vya Afya na ujenzi wa Hospitali hapa nchini hali ya upatikanaji wa huduma zimekuwa  bora na hata watumishi wa sekta ya Afya wanafanya kati zao katika mazingira bora ikilinganisha na siku za nyuma ambako kulikuwa na changamoto kubwa ya mazingira bora ya kazi.

Jackson Lugaraba na mfanyakazi wa  Hospiatli hiyo Dkt Rubi Mwita Marwa walisema, wamempongeza sana Rais Dkt John Magufuri kwa kazi mzuri ya kujenga miundombinu ya Afya na kwani imechochea hali ya wananchi kwenda katika vituo vya kutolea huduma pindi wanapoumwa na kuchochea uwajibikaji kwa watumishi wa sekta ya Afya.

Dkt Marwa alisema, ujenzi wa Hospitali ya halmashauri hiyo ambao uko katika hatua za mwishi kukamilika utachochea na kuongeza  hamasa kwa wafanyakazi katika suala zima la kutoa huduma mzuri kwa wananchi.

Afisa mipango wa Halmashauri hiyo Pastory Mgaruka alisema,Halmashauri  ilipokea shilingi bilioni 1.5 kutoka Serikali kuu na ilianza ujenzi wa Hospitali hiyo  katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019.

Alisema, kukamilika kwa Hospitali hiyo  kutasaidia wakazi  takribani laki moja na elfu arobaini wa halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe  kuondokana na hadha ya kutembea umbali mrefu hadi  Hospitali ya mkoa Mjini Mpanda kufuata baadhi ya huduma muhimu ikiwemo ya upasuaji ambayo haipatikani katika zahanati zilizokuwepo.

Mkaruka alisema,  ujenzi huo ulianza kutekelezwa kuanzia mwaka jana kwa gharama ya  biliioni 1.5  na mradi huo ni mkubwa  na kutakuwa na majengo ishirini na mbili ili kutengeza Hospitali ya wilaya ambapo  baadhi ya majengo yamekamilika na kuanza kutoa huduma na majengo mengine yatajengwa kwa awamu na katika bajeti ya  mwaka 2019/2020 wametenga milioni mia tano.

Alisema,  Hospitali hiyo ni kati ya miradi mikubwa inayojengwa na Serikali  katika Halmashauri hiyo ya Mpimbwe ambayo inalenga kusogeza,kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma mbalimbali jirani na kuwaondolea usumbufu wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma.

Alitaja miradi mingine iliyotekelezwa na kuanza kutoa huduma ni pamoja na ujenzi wa kituo cha Afya Husevya na Mamba ambayo imekamilika na imeanza kufanya ya kuwahudumia wananchi.

Alisema, Hospitali  hiyo  ni moja kati ya miradi mikubwa  saba inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mpimbwe, mingine ni ya sekta ya utawala,maji na elimu ambayo imekamilika na inafanya kazi.

Mganga mkuu wa Halmashauri hiyo Dkt Edward Sengo amemshukuru Rais Dkt John Magufuri kwa kuleta fedha  bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba katika Hospitali hiyo.

Alisema, kwa mwaka wa fedha 2020/21 wanategemea kupokea fedha milioni mia tano ambazo zitakwenda kukamilisha ujenzi  huo hata hivyo katika Hospitali hiyo wameshaanza kutoa baadhi ya huduma ikiwemo ya wagonjwa wan je(OPD) huduma za mama na mtoto na ushauri nasaha.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mpimbwe Erasto Kiwale alisema,katika bajeti ya mwaka 2020 wametenga jumla ya shilingi bilioni 1 ambazo zitatumika kujenga nyumba za watumishi ikiwemo  ya mkurugenzi na wakuu wa idara.

Aidha amemshukuru Rais Dkt John Maaguri kupeleka fedha katika halmashauri hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya  maendeleo ambayo imehamasisha wananchi kufanya kazi za kujiletea maendeleo na  kushiriki katika ujenzi wa Taifa kwa njia ya kujitolea.

Alisema,  Halmashauri imefanikiwa kuboresha miundombinu katika sekta ya elimu kwa kujenga vyumba vya madarasa,maktaba,nyumba za walimu,ofisi za serikali za vijiji na kata.