Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Suleiman Msuya kushoto akimkabidhi Bw John Bukuku Mkurugenzi wa Fullshangweblog na Fullshangwe tv Barakoa ambazo zimetolewa kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kutoka kiwanda Cha maziwa Cha ASAS Cha mkoani Iringa leo jiini Far es salaam.
………………………………………………………..
NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya ASAS imetoa msaada wa Barakoa (Masks) 1,000 kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari vya jijini Dar es Salaam ili waweze kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.
Msaada huo umetolewa na kampuni hiyo kwa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo Habari Tanzania (JOWUTA), ili kuwapatia wanachama wake na waandishi kwa ujumla.
Akizungumzia msaada huo Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya ASAS, Ahmed Salim alisema wameamua kusaidia kundi hilo kutokana na mchango wake kwa jamii katika kipindi hiki cha corona.
Mkurugenzi huyo alisema waandishi wa habari kazi zao zinahitaji kukutana na watu mbalimbali hivyo wanapaswa kuwa na vifaa vya kujikinga na maambukizi hivyo kampuni hiyo inaamini imetoa msaada sehemu sahihi.
“Nyie ni watu muhimu katika kuhabarisha jamii kuhusu maambukizi ya corona hivyo ni imani yetu kuwa Barakoa hizi 1,000 zitasaidia kwa muda na tutaendelea kushirikiana na JOWUTA kusaidia hali ikiruhusu,” alisema.
Salim alisema iwapo waandishi watapata maambukizi jamii itakosa taarifa sahihi za COVID-19, hivyo kuwataka wadau wengine kulisaidia kundi hilo muhimu kwa maendeleo ya nchi na wananchi.
Mkurugenzi huyo aliwaomba waandishi kuzingatia misingi, kanuni na sharia zinazosimamia taaluma yao kwa kuandika habari za kweli ili kutopotosha wananchi.
“Tumekuwa tukitoa misaada kama hii kwa makundi mbalimbali, hivyo basi sisi tunaamini nyie ni watu sahihi na mtazitumia kwa maslahi mapana ya kazi zenu kwa kuzingatia maadili,” alisema.
Alisema wametoa Barakoa, vitakasa mikono, mashine ya kupulizia mwili mzima, ndoo na vingine lengo likiwa ni kusaidia jamii ambayo kwa namna moja au nyingine inatumia malighafi za ASAS.
Akizungumzia msaada huo Katibu Mkuu wa JOWUTA, Suleiman Msuya alipongeza Kampuni ASAS kuwakumbuka waandishi wa habari wa Dar es Salaam ambao walikuwa wanapitia changamoto ya uhaba wa vifaa hivyo.
Msuya alisema waandishi wa habari walikuwa wanapata wakati mgumu wa kutafuta habari kutokana na mambukizi ya corona kusambaa jijini Dar es Salaam lakini kupitia msaada huo wa ASAS watakuwa wamepata suluhu kwa muda.
“Tunaishukuru Kampuni ya ASAS kwa msaada huu wa Barakoa 1,000 zitatusaidia sana katika kipindi hiki kigumu naamini sasa tutafanya kazi kwa uhuru na hata tukiandika habari na makala za kusisitiza uvaaji barakoa tunaonekana kwa mfano,” alisema Msuya.
Katibu huyo aliwataka waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kuzingatia maandili ya uandishi hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia wakati mgumu.
Msuya alitoa rai kwa waandishi wa habari kuepuka kutumika katika kipindi hiki kwani madhara yake yanaweza kuwa makubwa.