Home Mchanganyiko VITA YA CORONA BAKWATA MWANZA YAWAASA WENYE UWEZO KUSAIDIA WASIOJI

VITA YA CORONA BAKWATA MWANZA YAWAASA WENYE UWEZO KUSAIDIA WASIOJI

0

Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, alhaji Sheikhe Hasani Kabeke, akitoa mwongozo wa ibada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani wakati akizungumza na waandishi wa habari jana.Picha na Baltazar Mashaka

………………………………………………………………………………………………….

NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza

 BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza, katika kukabiliana na mamabukizi ya Virusi vya Homa kali ya Mapafu (Covid-19) limetoa mwongozo wa ibada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuwataka watu wenye uwezo kuwasaidia  vifaa vya usafi na vitakasa mikono, wasiojiweza na misikiti.

Pia limewataka wafanyabiashara kuacha kupandisha bei ya vyakula na bidhaa nyingine kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani ili kutowaumiza waumini wa dini ya Kiislamu na kuonya asitokee mtu akafanya kinyume.
Akizungumza na waandishi wa habari jana  jijini hapa kwa niaba ya Baraza la Ulamaa, na Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke ,alisema watu wenye uwezo na nafasi wawasaidie wasio na uwezo na  kutoa vifaa vya usafi kwenye misikiti ili watafute radhi ya Mwenyezi Mungu.
Pia alisema katika kujikinga na maambukizi ya corona, utaratibu wa kufutulisha kwa pamoja unaweza kuleta athari, hivyo umesitishwa na badala yake wenye nia ya kufutulisha watu wasio na uwezo waandae  vyakula vya kubeba mikononi ama wawagawie  wakapike wenyewe  ili kupunguza maambukizi.
“Baraza la Ulamaa limetoa maelekezo  namna  ya kuendesha ibada katika  kukabiliana na kujikinga na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (Covid-19), swala zote za Faradhi zisaliwe kwa ufupi ikiwemo Tarawehi kusomwa rakaa 10 badala ya 20 , hotuba misikitini pia zisichukue muda mrefu kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,”alisema Sheikhe Kabeke.
Aliwataka waumini wa dini hiyo kuvaa barakoa , watawaze nyumbani na waende na miswala yao wanapokwenda kuswali misikitini,wasishikane wala kukumbatiana na waachiane nafasi mita moja ikiwezakana yawekwe mahema nje ya misikiti  ikiwa ni njia ya kupunguza msongamano.
Sheikhe huyo wa Mkoa wa Mwanza, aliongeza kipindi hiki cha ukarimu na cha kujinyenyekeza kwa Mungu  Waislamu wote wakitumie  kutoa sadaka,misaada na kuomba toba jambo ambalo litasaidia kuondoa matatizo mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa Corona.
“Nitumie fursa hii kipekee kumshukuru Rais John Magufuli kwa msimamo usioyumba na kuruhusu nyumba za ibada kuendelea kutumika kwani hilo ndilo daraja la kutuvusha na maambukizi ya virusi vya Covid-19,”alisema.