Home Mchanganyiko DC DAQARRO ATOA WIKI TATU MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI

DC DAQARRO ATOA WIKI TATU MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI

0

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Gabriel Daqarro, aliyeweka mkono mfukoni akitoka kukagua ujenzi wa njia ya kuunganisha majengo katika kituo cha Afya cha Murieti jijini Arusha

……………………………………………………………………………….

Na Allan Isack,ARUSHA

MKUU wa Wilaya ya Arusha Mjini,Gabriel Daqarro, ametoa wiki tatu kwa kampuni ya ujenzi ya Surchet, kukamilisha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Sombetini jijini Arusha.

Daqarro alilitoa agizo hilo, jana wakati ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.

“Mkandarasi wa kampuni ya Surchet naagiza ndani ya wiki tatu hakikisha unakamilisha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na uyakabidhi kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Arusha,”alisema Daqarro.

“Lengo la ziara yangu ni kukagua mwenendeo wa ujenzi wa miradi ya maendeleo katika Jiji la Arusha, na mirani tuliyotembelea ni pamoja na miradi ya elimu, afya na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami,”aliongeza.

“Nitumie fursa hii kuupongeza uongozi wa shule ya sekondari ya Sombetini, shule hii kwa mwaka 2019, ilishika nafasi ya kwanza ngazi ya Wilaya, kwenye matokeo ya kidato cha nne, na ilifaulisha wanafunzi 147 kwenda kidato cha tano,”alisema.

Hata hivyo, alisema kukamilika kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo, kutapunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.

Licha ya kuzungumza hayo, alisema endapo ujenzi huo, utakamilika kwa wakati itasaidia wanafunzi kusoma na kuelewa wakiwa darasani.

Katika ziara hiyo, Daqarro, alitembelea mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Msingi Maweni Kata ya Terati,ujenzi wa madarasa manne ya ghorofa katika shule ya sekondari ya Arusha Terati na ujenzi wa njia za kuunganisha majengo kituo cha afya Muriet.

Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa madarasa manne ya ghorofa katika shule mpya ya Muriet B na matundu 10 vyoo, ujenzi wa barabara ya Oljoro kwenda Murieti kiwango cha lami na ujenzi wa barabara ya Sombetini kwenda FFU kwa kiwango cha lami.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk.Maulid Madeni, alisema mkandarasi huyo amelishapwa fedha zaidi ya sh.milioni 63, ili kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Aidha alisema kiasi cha fedha anazodai mkandarasi huyo, atalipwa na halmashauri hiyo baada ya kukamilisha ujenzi huo.