Home Mchanganyiko WATENDAJI SERIKALINI WAELIMISHWE KUTOA HAKI KWA WAKATI-RC MONGELLA

WATENDAJI SERIKALINI WAELIMISHWE KUTOA HAKI KWA WAKATI-RC MONGELLA

0

Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu (katikati) akiongea wakati alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella (kulia) ofisi kwake jijini Mwanza Aprili 20, 2020. Kushoto ni Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat Fatma Muya.

Afisa Mfawidhi wa Ofisi za THBUB Kanda ya Ziwa, Albert Kakengi (kushoto) akimuonesha Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat Fatuma Muya (Kulia) baadhi ya machapisho kuhusu haki za watoto yaliyopo katika maktaba ndogo ofisini hapo. Wa pili kulia ni Kaimu
Mkuu wa Kitengo Mipango wa THBUB, Laurent Burilo. Uongozi wa THBUB ulitembelea Ofisi hizo za Mwanza Aprili 20, 2020.

Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa THBUB Kanda ya Mwanza alipoitembelea Ofisi hiyo Aprili 20, 2020. Wapili kutoka kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat Fatuma Muya.

…………………………………………………………………………………….
Na Mbaraka Kambona,
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mh. John Mongella ameishauri Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kuandaa mpango maalamu wa kutoa elimu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa Watendaji wa ngazi za mikoa ili waweze kutoa haki za wananchi kwa wakati.
Mongella alitoa rai hiyo katika kikao kifupi kilichofanyika baina yake na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu alipomtembelea ofisini kwake jijini Mwanza Aprili 20, 2020.
Akiongea katika kikao hicho Mongella alisema kuwa kuna haja Tume kuweka utaratibu wa kutoa elimu kwa viongozi wa ngazi za mikoa kupitia vikao vyao vya kiutendaji ili kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya haki za binadamu na utawala bora na kujua wajibu wao.
“Ni vizuri mkaweka utaratibu kupitia vikao vya Watendaji Wakuu katika mikoa ili kuwaelimisha juu ya dhana nzima ya utoaji haki kwa wananchi, ni muhimu kuwaelimisha viongozi hawa kujua haki na wajibu wao, kwani bila kufanya hivyo matatizo hayo ya kutopata ushirikiano kutoka kwao yataendelea kuwa changamoto kwenu”, alisema Mongella.
Aliongeza kuwa taasisi za serikali hazina budi kufanya kazi kwa pamoja kwa sababu lengo lao ni kuhudumia wananchi, hivyo ni muhimu kupitia vikao hivyo vya watendaji Tume ikavitumia kuwaelimisha pia kujenga uhusiano utakao warahisishia utendaji kazi wake.

“Kuna wakati haki inachelewa kushughulikiwa na viongozi aidha kwa sababu ya uzembe au kwa kiongozi kutokujua wajibu wake katika kutoa haki hiyo ya mwananchi kwa wakati”, aliongeza Mongella
“Tunaweza tukawa tunapambana na matokeo wakati kabla ya matokea kuna chanzo. Tutoe elimu kwa viongozi, tukiweza kuwaelimisha vizuri naamini tutapunguza kushughulika na matokeo na malalamiko yatapungua”, alisisitiza

Akiongea mapema, Jaji Mwaimu alimueleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa nia ya Tume ni kuisaidia na kuijenga zaidi Serikali ili iweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi kwa kuzingatia haki za binadamu na utwala bora na njia pekee ya kufanya hivyo ni kwa Tume kushirikiana kwa karibu na taasisi nyingine za Serikali ambazo zinatoa huduma kwa wananchi.
Jaji Mwaimu aliendelea kusema kuwa ni vigumu kuhamasisha masuala ya haki za binadamu bila kuwahusisha wadau ambao kwa kiasi kikubwa ni Serikali.

Jaji Mwaimu alikutana na Mongella ikiwa ni sehemu ya ziara yake jijini Mwanza ambayo lengo lake kubwa ni kutembelea ofisi za Tume zilizopo kanda ya Ziwa ili kushughulikia malalamiko ya wananchi yaliyowasilishwa katika ofisi hizo.