************************************
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Wakulima wengi ndani ya Tarafa ya Mihambwe wamehamasika mwaka huu kulima zao la Ufuta kutoka kwenye utegemezi wa zao moja la biashara la Korosho.
Wakulima hao wakizungumza wakati wa ziara aliyoifanya Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu wameishukuru Serikali ya Rais Magufuli kwa kuwahamasisha, kuwapatia pembejeo kwa wakati na kuhakikisha upatikanaji wa masoko kwa wakati.
“Sisi Wakulima tunaishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli kwa kutupatia hamasa, elimu, mbegu na masoko ndio maana siku hadi siku tunazidi kuhamasika kulima Ufuta badala ya kutegemea zao la biashara la Korosho pekee. Ufuta unalipa sana, unatuinua kiuchumi Wakulima.” Alisema Mkulima Ayoub Abrahaman Dabi wa Kijiji cha Michenjele kata ya Michenjele aliyelima hekta 15 za Ufuta mwaka huu.
Gavana Shilatu akizungumza mara baada ya ziara yake alieleza matarajio ya upatikanaji wa Ufuta mwaka huu ni mkubwa zaidi kutokana na Wakulima wengi kujitokeza kulima zao hilo la biashara.
“Haikuwa kazi rahisi kubadili fikra za Wakulima waliokuwa wakitegemea zao moja la biashara la Korosho. Katika msimu wa mwaka huu ndani ya Tarafa ya Mihambwe tunatarajia kupata mavuno ya zaidi ya tani 150 kutoka mavuno ya tani 70 ya msimu uliopita. Ni hatua kwetu katika historia ya kilimo cha Ufuta kwa kipindi kifupi tu cha miaka 2.” alisema Gavana Shilatu.
Katika ziara hiyo ya kutembelea na kujionea hali ya Ufuta ndani ya Tarafa ya Mihambwe, Gavana Shilatu aliambatana na Maafisa Ugani, Watendaji Vijiji pamoja na Viongozi wa Serikali za Vijiji.