Home Mchanganyiko TAKUKURU MANYARA YAWATIA MBARONI WENYEVITI KWA RUSHWA YA CORONA

TAKUKURU MANYARA YAWATIA MBARONI WENYEVITI KWA RUSHWA YA CORONA

0

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.

……………………………………………..
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoani Manyara, inawashikilia wenyeviti wawili wa serikali ya kijiji na kitongoji Wilayani Simanjiro kwa kudaiwa kuomba rushwa ya sh35,000 ili wakazi watano wa eneo hilo waliorudi kutoka nchi za nje wasikae karantini.

Wenyeviti hao wa serikali ya kijiji cha Ngage, kata ya Loiborsoit, Andrea Daniel na Mwenyekiti wa kitongoji kwa Ngage B, Letapuka Kuyani wanadaiwa kupokea rushwa ya sh38,000 kwa kila mkazi wa eneo hilo anayetoka nje ya nchi ili wasikae karantini ya siku 14.

Mkuu wa Takukuru mkoani Manyara, Holle Makungu akizungumza jana alisema viongozi hao wanadaiwa kupokea rushwa kinyume na sheria wakati huu ambapo serikali ipo katika kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

Makungu alisema viongozi hao wa kijiji na kitongoji wamekuwa wakichukua sh35,000 kwa kila mkazi wa eneo hilo atakayetoka nje ya nchi ikiwemo Zambia, Kenya na Uganda ili wasikae karantini.

Alisema viongozi hao huchukua kiasi hicho cha fedha kwa wananchi wa eneo hilo wanaotoka nje ya nchi ili wawaruhusu wakalale kwenye maboma ya jamii ya wafugaji badala ya karantini.

Alisema uchunguzi wao umebaini kuwa wakazi wa eneo hilo wakiingia nchini hutakiwa kuwekwa karantini kwa siku 14 ili wakapimwe maambukizi ya corona ila hutoa rushwa na kuruhusiwa kwenda kwenye maboma yao.

“Pia wale ambao wamewekwa karantini kutozwa rushwa ya sh28,000 na viongozi hao wakidai kuwa ni gharama za madaktari na mafuta ya magari kwa siku 14 za kuwekwa karantini,” alisema Makungu.

Alitoa wito kwa viongozi wa maeneo mbalimbali kwenye mkoa huo kuacha tamaa ya fedha na kuungana na serikali katika kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.

“Wananchi wanapopata taarifa ya kuwepo kwa mtu ambaye alikaa nje ya nchi na kuingia nchini bila kukaa karantini wanapaswa kufikisha sehemu husika ili kupambana na maambukizi ya virusi vya corona,” alisema Makungu.