Home Mchanganyiko MTATURU AMSHUKURU RAIS MAGUFULI KWA KUTOA SH BILIONI 2 ZA UJENZI WA...

MTATURU AMSHUKURU RAIS MAGUFULI KWA KUTOA SH BILIONI 2 ZA UJENZI WA VETA IKUNGI

0

…………………………………………………………………..

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amekagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha ufundi stadi (VETA)kinachojengwa Wilayani Ikungi na kuridhishwa na hatua iliyoanza katika ujenzi huo.

Chuo hicho kinajengwa katika kijiji cha Muungano kata ya Unyahati ambapo serikali ilitoa Sh Bilioni mbili lengo likiwa ni kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa fani mbalimbali.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo ambao upo katika hatua za awali za kuanza kuchimba msingi na kusogeza vifaa,Mtaturu amewapongeza kwa uharaka wao na kuwataka kuhakikisha fursa za ajira zisizo na ujuzi zitakazopatikana ziwahusishe vijana wa Ikungi ili nao wapate kipato na wafaidike na mradi kuwa karibu nao.

Amesema ujenzi huo umetokana na ombi walilolitoa kwa Mhe Rais Dkt John Magufuli baada ya utafiti walioufanya kuonyesha kuwa asilimia 20 ya vijana wanaomaliza kidato cha nne ndio wanaoendelea na masomo ya juu na asilimia 80 wanabaki nyumbani kwa kushindwa kujiajiri na kuwa mzigo kwa familia.

“Mhe Rais baada ya kupokea ombi letu aliridhia kutoa Sh Bilioni 2 ili ujenzi huu uanze,nichukue fursa hii kumshukuru sana kwa upendo wake wa kuwasaidia watoto wa wanyonge wapate elimu itayowasaidia kujikwamua kiuchumi,”alisema Mtaturu.

Amesema lengo lao ni kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ndani ya miezi sita ili wanafunzi wadahiliwe kwa mwaka unaokuja wa masomo.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Veta Singida Paul Batoleki amesema ujenzi huo unaenda kwa awamu na awamu ya kwanza wanatarajia kujenga msingi mfuto wa majengo saba na jengo la nane la utawala litakamilika ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.

“Hapa tunatumia mfumo wa “force account” ambao unatumia pesa kidogo kwa kazi kubwa,majengo yanayotarajiwa kujengwa ni Utawala,Darasa la Jumla,Karakana ya Ushonaji,Darasa la Uhazili na Kompyuta,Karakana ya Umeme na Uchomeleaji Vyuma, Karakana ya Magari,Jiko na Bwalo la Chakula na Mabweni mawili la Wavulana na Wasichana na Uwekaji wa Samani,”alisema Mkuu huyo wa Chuo.

Nae Diwani wa kata ya Unyahati Abelly Surry amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwapelekea mradi huo muhimu kwa jamii.

“Nikushukuru pia na wewe mbunge kwa kutusemea kwa Mhe Rais tangu ukiwa  Mkuu wa Wilaya hadi sasa mradi unaanza,haya ni maono yenu na tunaahidi kuendelea kuwaunga mkono ili  mradi huu uwe chachu ya maendeleo kwenye kata na wilaya kwa ujumla,”alisema Diwani huyo.