Home Mchanganyiko MAHAKAMA YAANZA UJENZI WA MAJENGO SITA YA VITUO JUMUISHI VYA UTOAJI HAKI...

MAHAKAMA YAANZA UJENZI WA MAJENGO SITA YA VITUO JUMUISHI VYA UTOAJI HAKI NCHINI

0

******************************

Na Lydia Churi-Mahakama

Mahakama ya Tanzania imeanza ujenzi wa majengo sita ya vituo Jumuishi vya utoaji haki katika mikoa mitano nchini ikiwa ni hatua ya Mhimili huo ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

 

Mkuu wa Kitengo cha Kusimamia Maboresho ya Mahakama (JDU) Mhe. Zahra Maruma amesema majengo hayo yameanza kujengwa kuanzia mwezi Januari mwaka huu na yanatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 10.

 

Alisema majengo hayo yatakuwa na sakafu nne yaani gorofa 3 na yatajumuisha ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama Kuu mpaka Mahakama ya Mwanzo pamoja na ofisi za baadhi ya wadau wa Mahakama wakiwemo Polisi, Ustawi wa Jamii, Mawakili na Waendesha Mashitaka.

 

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Kusimamia Maboresho ya Mahakama, majengo hayo yameanza kujengwa katika miji ya Arusha, Mwanza, Dodoma,
Morogoro na Dar es Salaam katika wilaya za Kinondoni pamoja na Temeke.

 

Kusudi la kuweka ngazi zote za Mahakama ndani ya jengo moja pamoja na ofisi za wadau ni kurahisisha na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za utoaji haki pamoja na kumpunguzia mwananchi gharama za kufuatilia huduma hizo katika ofisi tofauti ambapo humlazimu mwananchi kutumia rasilimali fedha na rasilimali muda katika kufuatilia huduma hizo.

 

Upatikanaji wa huduma shirikishi katika majengo haya kutampatia mwananchi fursa ya kutumia muda mchache wa kupata huduma na kumuongezea muda wa kujishughulisha katika shughuli za uzalishaji
na kijamii. badala ya kutumia muda huo kuzunguka katika ofisi tofauti kupata huduma za haki.

 

Majengo haya yanajengwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa Maboresho ya Huduma za utoaji haki wa kipindi cha
miaka mitano ( Citizen – Centric Judicial Modernisation of Justice Service Delivery). Lengo la Mahakama ya Tanzania ni kuhakisha kunakuwepo na Mahakama Kuu katika kila mkoa, Mahakama za Hakimu Mkazi katika kila Mkoa,
Mahakama za Wilaya kwenye kila Wilaya na Mahakama za Mwanzo kwenye kila Tarafa kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.