Mkurugenzi Mkuu wa AFRICAB Mansoor Moiz
UWEPO wa biashara ya mabomba ya plastiki (PVC) yasiyo na ubora katika soko nchini kwa kiasi kikubwa kumetajwa kuchangiwa na baadhi ya wenye viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo kutozingatia sheria sambamba na waagizaji wasio wa nje ya nchi wasio waaminifu.
Hatua hiyo pamoja na mambo mengine imebainishwa kuwa moja ya sababu kuu ya wananchi kupata hasara mbalimbali hususani pale linapotokea bomba hilo kupasuka na kusababisha athari katika njia za umeme na wakati mwingine hata kusababisha kuungua kwa nyumba na miundombinu mingine ya umeme.
Kimsingi mabomba hayo(PVC), huzalishwa maalumu kwa ajili ya matumizi ya usafirishaji wa nyaya za umeme katika ujenzi wa nyumba na majengo mengine lakini pia miundombinu inayotekelezwa katika miradi mbalimbali ikiwemo ya majengo na umeme nchini.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha utengenezaji wa vifaa vya umeme cha Kilimanjaro Cables (AFRICAB) kinachozalisha mabomba ya PVC maalumu kwa ajili ya usambazaji wa umeme Mansoor Moiz, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusiana na uzalishaji wa bidhaa hizo wanaoufanya
Kwa mujibu wa Mansoor, Tanzania inapiga hatua kubwa katika uzalishaji wa mabomba hayo, isipokuwa kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya wenye viwanda hivyo kuzalisha bidhaa zisizo na ubora.
Alisema uzalishwaji huo wa mabomba yasiyo na ubora unaotakiwa kulingana na viwango vya TBS, kimsingi umekuwa ukisababisha athari katika soko na kwamba imekuwa ngumu kuwabaini wahusika wa bidhaa hizo kwa kuwa hawajitambulishi katika bidhaa hizo kama watengenezaji.
“Kujenga jina ya kampuni inachukua maisha lakini kwa mara moja unaweza kuanguka, tunapaswa kuzingatia ubora wa bidhaa zetu kulingana na matakwa ya Shirika la Viwango Tanzania(TBS),ni wajibu wetu kuwa waminifu kwa Serikali yetu, kama wazalishaji wote tujifanya hivyo wazi kuwa tutaepusha athari kwa watanzania wenzetu ikiwemo kuokoa nyumba zao kuungua, fedha na hata maisha yao kwa ujumla” alisema Mansoor
Alisema kimsingi kazi ya usambazaji wa nyaya ‘cables’ maeneo tofauti ikiwemo chini ya ardhi inahitaji mabomba yenye viwango vya kutosha na teknolojia ya hali ya juu, tofauti na hivyo mabomba hayo yanaweza kupasuka na kusababisha madhara yasiyo tarajiwa huku akiwataka wenye viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo nchini kote kuifanya kazi hiyo kwa ushirikiano wa pamoja na weledi .
“Ni muhimu tushirikiane kwa pamoja katika suala hili, tujivunie nchi yetu na viwanda vyetu huku tukijua kuwa kuzalisha bidhaa zisizo na ubora ni kuwaumiza wananchi wenzetu na kulikosea heshima taifa letu ambalo katika uongozi huu chini ya Rais John Magufuli limetupa fursa kubwa ya kuwekeza katika viwanda” aliongeza Mansoor
Hivi karibuni Rais John Magufuli alitoa rai kwa wenye viwanda hao kuhakikisha wanazalisha bidhaa zenye ubora pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwa na bei ya chini ya bidhaa hizo ili kulinda soko la ndani sambamba na kumwezesha mwananchi kumudu.
Alisema ni ajabu kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kuwa na bei ya ghali zaidi ya zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi na kuhoji nini sababu ya viwanda hivyo kuwa na bei ya juu katika bidhaa hizo wakati hazilazikiki kusafirishwa kutoka nje ya nchi.