Home Mchanganyiko TAKUKURU MKOA WA DODOMA YAOKOA SHS. 297,115,474 NA KUSHIKILIA MAGARI MATATU

TAKUKURU MKOA WA DODOMA YAOKOA SHS. 297,115,474 NA KUSHIKILIA MAGARI MATATU

0

………………………………………………………………………………………………..

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kushirikisha ofisi zake zote za wilaya na wananchi kwa ujumla, ambapo kwa robo ya Januari hadi Machi, 2020 imetekeleza mambo mengi na hii ni taarifa ya baadhi ya mambo hayo: 

Ufuatiliaji wetu katika Miradi ya Maendeleo umewezesha mradi wa maji wa kijiji cha Mlongia wilayani Chemba kutoa maji na kuwafaidisha wananchi zaidi ya elfu tano ambao awali hawakuwa na huduma ya maji safi. 

Mradi huo wenye thamani ya shilingi 579,323,000/= ulianza mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2014 lakini haukuwa unatoa maji hadi tulipofuatilia na Mkandarasi ambaye ni LeoStart Engineering Co. Ltd kurudi katika eneo la mradi na kufanya marekebisho na sasa maji yanatoka. Ufuatiliaji wetu ulibaini pamoja na mradi kuwa chini ya kiwango, pia Mkandarasi alilipwa shilingi 120,247,164 zaidi ya thamani ya kazi zilizofanyika hivyo pamoja na kurekebisha mradi ili utoe maji tayari ameanza kurejesha Serikalini fedha alizozidishiwa. 

Tunaendelea kufuatilia utokaji wa maji na kuhakikisha Mkandarasi anarejesha kiasi cha fedha kilichosalia. 

Aidha, katika kipindi tajwa tumeokoa jumla ya shilingi 297,115,474 pamoja na kushikilia magari matatu kutokana na ufuatiliaji wa kazi mbalimbali ili kuhakikisha fedha na mali za 

umma zinatumika kulingana na taratibu sahihi na sio kufujwa. 

Shilingi 143,515,177 ziliokolewa kutoka kwa viongozi na wanachama 67 wa vyama sita vya akiba na mikopo (Saccos) waliokuwa wanadaiwa kwa muda mrefu, na; Magari matatu aina ya Toyota Hiace yalichukuliwa kutoka kwa viongozi wa Saccos moja waliokuwa wanayatumia kwa faida binafsi. Ufuatiliaji wa madeni na 

mali za ushirika ni utekelezaji wa agizo la serikali la kuhakikisha fedha na mali za wananchi zinarejeshwa sehemu stahiki. Kiasi kilichobaki cha shilingi 153,600,297 kimeokolewa kwa kufuatilia na kurejesha mapato ya serikali yaliyokusanywa kwa njia ya kieletroniki (POS) lakini hayakuwasilishwa sehemu husika; fedha za vitambulisho vya wajasiriamali; mishahara hewa; matumizi yaliyofanyika kinyume na maelekezo; fedha zilizochepushwa kutoka katika miradi ya maendeleo; na malipo zidifu kwa wakandarasi katika miradi ya maji Mlongia na Kelema kuu. Pia tumefuatilia na kukagua miradi ishirini na sita (26) ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya shilingi 6,611,512,391 katika sekta za elimu, maji, ujenzi, 

mo na umwagiliaji, mapato na utawala, ambapo jumla ya shilingi 94,779,950 zimeokolewa baada ya kuwa zimechepushwa katika miradi hiyo na hivyo kuongeza ufanisi wa utekelezaji wake. Vilevile, ufuatiliaji wetu katika miradi hii umebaini kuwa miradi minne yenye thamani ya jumla ya shilingi 261,042,561 ina viashiria vya rushwa na udanganyifu 

hivyo tunaichunguza. Ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo una faida kubwa kwani pamoja na kuokoa rasilimali zinazochepushwa, unasaidia miradi hiyo kukamilika kwa wakati na kwa viwango stahiki. Lakini zaidi ufuatiliaji huo unachochea ushiriki wa wananchi katika kuisimamia. 

Tumefanya uchambuzi wa mifumo ya utendaji na utoaji huduma katika maeneo yafuatayo: 

– Vyama vya ushirika, Fedha, Michezo na Maliasili. Lengo la uchambuzi huu ni kubaini mianya ya rushwa, na tumefanya vikao sita vya kiutendaji kujadili na wadau, wa fedha na vyama vya ushirika, taarifa zetu za uchambuzi wa mifumo na kuwekeana maazimio ya kuondokana na mianya iliyobainika. 

Aidha, tulifuatilia utekelezaji wa mikakati tuliyowekeana huko nyuma na wadau katika sekta za ardhi, elimu na mapato ili kuhakikisha kwamba vikao vya kiutendaji tunavyokaa na mikakati ya kuondoa rushwa tunayoiweka inatekelezwa kwa wakati ili kuondoa kero ya rushwa na kuongeza tija katika utendaji na utoaji huduma. 

Ndugu Waandishi wa Habari, Ni wajibu wetu kuushirikisha umma katika juhudi za kuzuia na kupambana na rushwa kwani bila ushiriki wa dhati wa watu wote – mapambano haya hayataleta tija inayokusudiwa. 

Tumeendelea kutumia mbinu za kuelimisha kupitia mikutano ya hadhara, semina, vipindi vya redio na maonesho, ambapo watu wa kada na rika mbalimbali wameelimishwa hasa katika maeneo ya kuikataa na kutoa taarifa dhidi ya vitendo vya rushwa ya ngono na elimu ya madhara ya rushwa katika uchaguzi. Vilevile tumeelimisha kuhusu umuhimu wa kukataa na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa ujumla. Kabla ya masomo katika shule na vyuo kusimamishwa, tulifungua klabu za wapinga rushwa katika shule 28 za msingi na sekondari na kuimarisha jumla ya klabu 70. Tunafanya hivi kwa kuamini kwamba vijana ni jeshi muhimu sana katika kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa. Ndiyo maana baadhi yenu mlishuhudia tukio la kitaifa ambalo lilifanyika katika mkoa wetu Februari 2020, 

ambapo TAKUKURU ilizindua Mkakati rasmi wa kushirikiana na Vijana wa Skauti katika kuzuia na kupambana na Rushwa nchini. Uelimishaji uliofanyika umechangia kupokelewa kwa taarifa mia moja thelathini na moja (131) za vitendo vya rushwa na makosa yahusianayo, ambapo kwa mujibu wa taarifa hizo, sekta zilizoongoza ni: Serikali za Mitaa (asilimia 38.9); Ardhi (asilimia 24.4); Vyama vya Ushirika (asilimia 8.4); Mahakama (asilimia 6.1); na Serikali Kuu (asilimia 5.3). Ni vyema kwamba viongozi na watumishi wa maeneo yanayoonekana kuongoza kwa kulalamikiwa wachukue hatua mapema ikiwa ni pamoja na kuimarisha mikakati yao ya ndani ya kudhibiti rushwa. 

Taarifa zisizohusiana na rushwa zilihamishiwa idara husika, na tulikamilisha uchunguzi wa majalada 21 na kufungua mashauri 19 mahakamani. Mashauri matatu yalitolewa uamuzi na mahakama ambapo Jamhuri imeshinda yote. 

Ndugu Waandishi wa Habari, Katika robo ya Aprili hadi Juni, 2020 TAKUKURU Mkoa wa Dodoma itaendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki kivitendo katika kuzuia rushwa na tutaendelea kutoa elimu ya rushwa kwenye uchaguzi. Aidha tutaendelea kufuatilia madeni ya vyama vya ushirika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana. 

Tunaendelea kuwaasa wananchi wote wa mkoa wetu wa Dodoma kuwa makini na watu wanaowapigia simu wakijifanya Maafisa wa TAKUKURU au idara nyingine za Serikali kwa lengo la kuwarubuni na kwamba kamwe wasikubali kutuma fedha kwa matapeli hao bali watoe taarifa mapema katika ofisi zetu kwa msaada zaidi. 

Pia tunawataka wale ambao tumewafikisha mahakamani kwa makosa mbalimbali kuacha tabia ya kuwafuata na kuwarubuni mashahidi wa Jamhuri kwani hilo ni kosa la jinai na tukiwabaini tutachukua hatua stahiki. 

Ninatambua na kushukuru sana mchango wa Vyombo vya Habari katika mkoa wetu wa Dodoma ambao siku zote mmekuwa mstari wa mbele kutoa fursa za kuelimisha dhidi ya rushwa na pia kuuhabarisha umma juu ya jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuzuia na kupambana na rushwa ndani ya mkoa wetu.