Home Mchanganyiko Wabunge Waweka Siasa Pembeni na Kupambana na Corona

Wabunge Waweka Siasa Pembeni na Kupambana na Corona

0

*****************************

Na Jonas Kamaleki, Dodoma

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameweka nguvu zao pamoja kupambana na ugonjwa wa Corona na kuweka itikadi zao za kisiasa pembeni.

 

Akizungumza leo Bungeni jijini Dodoma katika kikao cha kwanza cha Bunge la Bajeti la 2020/21, Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai amewataka wabunge na wadau wengine
waweke umbali kati ya mtu na mtu (sociali distance) ili kuepuka maambukizi ya Corona.

 

Kwa kuzingatia hilo, jumla ya wabunge wasiozidi 150 ndio wanaoruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa Bunge. Muda wa vikao vya Bunge nao umebadilishwa na kufanya vikao vya bunge hilo kuanza saa 8:00 alasiri hadi saa 12:00 jioni badala ya saa 3:00 asubuhi.

 

Baadhi ya wabunge waliofanya mahojiano na Idara ya Habari (MAELEZO) wameonyesha kuondoa tofauti zao za vyama, itikadi na mitazamo na kuweka nguvu ya pamoja
kupambana na Corona.

 

Mhe. Joseph Selasini (Mb) Rombo CHADEMA amesema anamuunga mkono Spika asilimia 100 na kuongeza kuwa mbunge au mtu yeyote anayefanya siasa katika janga hili huyo atakuwa na upungufu wa kifikira.

 

“Ugonjwa huu ukisambaa utamkumba mwanasiasa wa chama chochote, mfanyabiashara wa aina yoyote na mwananchi wa mazingira yoyote”, amesisitiza Mhe.
Selasini.

 

Akitoa maoni yake kuhusu vita dhidi ya Corona, Mbunge wa Mbozi CHADEMA, Paschal Haonga amesema ugonjwa wa Corona hauna itikadi unaweza kumpata mtu yeyote yule na kuwataka wautambue ugonjwa huo kuwa ni adui wa kila mtu.

 

Aidha, amewahimiza watu wote wanaouza vifaa vya kujikinga na ugojwa huo kupunguza bei ili wananchi wa kawaida waweze kumudu gharama za upatikanaji wa
vifaa hivyo na kupunguza kasi ya maambukizi na kusambaa kwake.

 

Naye Anthony Komu, Mbunge wa Moshi Vijijini CHADEMA anasema, “Tuungane pamoja kama viongozi wa nchi kupambana na janga la Corona bila kujali vyama vyetu vya
siasa”. Amewaasa viongozi wenzake wawe makini katika kufuata masharti yanayoelezwa na wataalaam katika kupambana na ugonjwa huo.

 

Kwa upande wake Rhoda Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum Katavi, CHADEMA amesema ugonjwa wa Corona si suala la kisiasa na ametoa wito kwa watanzania na Serikali kwa ujumla kuweka vituo vya kupima ugonjwa huo hususan kwa watu wanaofanya kazi katika masoko makubwa kama Kariakoo na ameiomba Serikali kupeleka vitendea kazi vya kupima ugonjwa huo maeneo mengi ya nchi ili kuepusha maambukizi mapya.

 

Naye Aida Kenani, Mbunge wa Viti Maalum Rukwa CCM ameitaka jamii ya watanzania kuacha mizaha na ugonjwa wa Corona na kuweka siasa kando kwa vitu vya msingi ili
taifa na maisha ya watanzania yapewe kipaumbele.

 

Bunge la Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2020/21 limeanza leo jijini Dodoma na linafanyika kwa aina tofauti na mikutano iliyopita, hatua hiyo inatokana na uwepo wa
ugonjwa wa Corona, ndiyo maana wabunge wachache wanaruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa bunge ambapo vikao hivyo vitafanyika kwa saa nne tu kwa siku.