Home Mchanganyiko Dkt. Ndungulile apongeza kukamilika kwa ujenzi hospitali ya Wilaya ya Kibaha.

Dkt. Ndungulile apongeza kukamilika kwa ujenzi hospitali ya Wilaya ya Kibaha.

0

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile akitoa maagizo alipotembelea Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mjini.

**************************************

Na WAMJW- Pwani.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile amepongeza wataalamu wa afya mkoani Pwani kwa kukamilisha ujenzi wa Hospitali mpya ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mjini ambayo kwa sasa itatumika kulaza wagonjwa watakaobainika kuwa na maambukizi ya homa ya Corona.

Dkt. Ndungulile ameyasema hayo wakati alipotembelea hospitali hiyo na kuwataka wataalamu kujipanga vizuri ili kukabiliana na ugonjwa huo hasa ikizingatiwa Wilaya ya Kibaha Mjini ni lango kuu la wageni kuingia jijini Dar es Salaam.

“Kibaha ni lango kuu la kuingilia Dar es Salaam, hivyo mnatakiwa kuchukua hatua madhubuti ya kuzuia maambukizi ya homa ya Corona,” amesema Dkt. Ndungulile.

Hospitali hiyo mpya imejengwa kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa wananchi na itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 40, lakini kwa sasa itatumika kuhudumia wagonjwa watakaobainika kuwa na maambukizi ya homa ya Corona.

Dkt. Faustine Ndungulile amewaagiza pia wataalamu wa afya mkoani Pwani kwenda katika maeneo ya ibada, vituo vya mabasi na sokoni kutoa elimu ya kupambana na homa ya virusi vya Corona.

Katika hatua nyingine, Dkt. Ndungulile amewataka kukamilisha miundombinu ya ndani na nje kwa kuweka uzio pamoja na mfumo wa maji.

Dkt. Ndungulile amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Gunini Kamba kupeleka vitanda 30 katika jengo ambako watalazwa wagonjwa watakaobainika kuwa na maambukizi ya homa ya Corona.

“Ujenzi wa Hospitali hii umekamilika, sasa hakikisheni mnakamilisha mfumo wa maji na kuweka vitanda katika jengo ambalo watalazwa wagonjwa wa homa ya Corona endapo itabainika kuwa na homa hiyo,” amesema Dkt. Ndungulile.