Home Mchanganyiko DKT. MPANGO ATAHADHARISHA WAFANYAKAZI KUJIKINGA NA CORONA NA KUTAKA IFANYIKE TATHIMINI YA...

DKT. MPANGO ATAHADHARISHA WAFANYAKAZI KUJIKINGA NA CORONA NA KUTAKA IFANYIKE TATHIMINI YA ATHARI ZA UGONJWA HUO KIUCHUMI

0

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Mary Maganga wakionesha namna ya kusalimiana wakati wa Mkutano na Watumishi wa Wizara hiyo (hawapo pichani) kuhusu tahadhari ya Virusi vya Corona vinavosababisha ugonjwa wa COVID- 19, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango-Treasury Squire, jijini Dodoma, tarehe 16 Machi, 2020.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akizungumza na Jumuiya ya Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mapango na kuwataka wazingatie kanuni bora za Afya ili kujikinga na Virusi vya Corona, tarehe 16 Machi, 2020, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage-Treasury Squire, Jijini Dodoma.

Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakichukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa COVID- 19 unaosababishwa na Virusi vya Corona kwa kunawa mikono kwa kutumia kemikali maalum (Sanitizer), katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango, Treasury Squire, Jijini Dodoma, tarehe 16 Machi, 2020.   

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga, akizungumza na Watumishi wa Wizara hiyo kuhusu kujikinga na Virusi vya Corona vinavosababisha ugonjwa wa COVID- 19 ambapo amewataka wajiuepushe na mikusanyiko isiyo ya lazima, tarehe 16 Machi, 2020, Jijini Dodoma

Afisa Utumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Tumwesige Kazaura, akitoa maelekezo ya namna ya kunawa mikono ili kujikinga na Virusi vya Corona, katika ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma, tarehe 16 Machi, 2020

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Michael, akisisitiza jambo wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kushoto), na watumishi wake (hawapo pichani), jijini Dodoma, tarehe 16 Machi, 2020;

Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakisikiliza maagizo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) kuhusu namna ya kujikinga na maambukizi ya Virus vya Corona, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma tarehe 16 Machi, 2020.

Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Fedha na Mipango (Viti vya mbele) wakisikiliza kwa makini maagizo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) kuhusu namna ya kujikinga na Virus vya Corona, katika ukumbi wa Kambarage, Jengo la Treasury Square, Jijini Dodoma, 16 Machi, 2020.

(Picha na Peter Haule, WFM, Dodoma)

*********************************

Na. Farida Ramadhani na Saidina Msangi, WFM, Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, amewaagiza Wataalamu wa Wizara hiyo kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuangalia madhara ya Corona yanayoweza kujitokeza katika uchumi wa nchi pamoja na namna ya kukabiliana nayo.

Agizo hilo amelitoa jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo kuhusu umuhimu wa kujikinga na Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa hatari wa COVID-19.

“Nilikuwa naangalia taarifa ya Tume ya Uchumi ya Afrika “Economic Commission of Africa” inayoelezea madhara ya ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa na Virusi vya Corona, kwa kweli inatisha, wanasema uchumi wa Africa unaweza ukaanguka na kufikia asilimia 1.8, wastani huwa ni asilimia 3.2”, alisema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango alisema kuwa ugonjwa huo ni hatari ni vema Taifa liandaliwe upande wa uchumi ili kujiweka sawa ma kutafuta namna ya kuchukua hatua katika kukabiliana na madhara yanayoweza kutokea kiuchumi hususani kwenye biashara na utalii.

Aliwataka Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo kwa kuzingatia taratibu za afya katika maeneo ya kazi na kwenye familia zao.

“Kila mmoja ana wajibu binafsi, wajibu katika familia na wajibu kazini ili tuendelee kukaa salama. Sitapenda kupoteza mtumishi hata mmoja wala mtumishi kupoteza mwanafamilia wake kutokana na ugonjwa huu”, alisema Dkt. Mpango.

Aliwaasa watumishi kuchukua tahadhari kwa kuiga mfano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, wa kuacha mazoea ya kushikana mikono wakati wa kusalimiana.

“Kiafrika unaonekana unaringa kweli usipompa mtu mkono, lakini kwa dharura tuliyonayo, muwafundishe na watoto wenu hakuna kupeana mikono” alisisitiza Dkt. Mpango. 

Alifafanua kuwa katika kupambana na ugonjwa huo, Wizara imeweka Kemikali maalum ya kunawia mikono (Sanitizer) inayoweza kuua vijijidudu kwenye maeneo mbalimbali ya Majengo ya Wizara hiyo, hivyo aliwataka watumishi wahakikishe wanaitumia wakati wanapoingia ofisini na kwa wenye uwezo wainunue kwa ajili ya matumizi ya familia zao.

Aidha, Aliwataka watumishi hao kutoa elimu ya afya kwa familia zao pamoja na kuepuka mikusanyiko na safari zisizokuwa za lazima za ndani na nje ya nchi ili kujikinga na ugonjwa huo.

Alisema ugonjwa huu ni kama vita na kwasasa kwani umeshafika katika nchi jirani za Kenya na Rwanda, hata hivyo alibainisha kuwa, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Wizara ya Afya, Tanzania iko salama.