Mwakilishi wa kikundi cha wakinamama 120 wanaojihusisha na uzalishaji wa kokoto katika eneo la Ntyuka jijini Dodoma, Blandina Daudi akielezea shughuli zinazofanywa na kikundi hicho kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini mara ilipofanya ziara katika machimbo ya mawe ya Ntyuka tarehe 12 Machi, 2020
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (katikati) akifafanua jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwenye machimbo ya
mawe ya Ntyuka jijini Dodoma tarehe 12 Machi, 2020. Kushoto ni Waziri wa Madini, Doto Biteko
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (kushoto) akitoa maelekezo kwa Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Laurent Bujashi (kulia)
wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika machimbo ya mawe ya Ntyuka tarehe 12 Machi, 2020.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (wa pili kushoto) akitoa
maelekezo kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (katikati)
wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika machimbo ya mawe ya Ntyuka tarehe 12 Machi, 2020. Kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula.
**************************
Na Greyson Mwase, Dodoma
Machi 12, 2020
Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini inaendelea kuhakikisha inawawezesha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili waweze kuwa mamilionea huku Serikali ikipata mapato yake kutokana na kodi mbalimbali na kuinua Sekta ya Madini.
Waziri Biteko aliyasema hayo leo tarehe 12 Machi, 2020 kwenye ziara ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanyika katika machimbo ya mawe ya nakshi Ntyuka,
Soko la Madini Dodoma na Chuo cha Madini Dodoma (MRI) yenye lengo la kufahamu utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Madini na Tume ya Madini.
Katika ziara hiyo, Waziri Biteko aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.
Alisema kuwa, ili kuhakikisha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini wanaendesha shughuli zao kwa faida, Serikali imeweka mazingira mazuri ikiwa ni
pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini nchini na kupunguza kodi mbalimbali.
Akielezea mikakati ya kuboresha masoko ya madini nchini yaliyoanzishwa tangu mapema Machi mwaka jana Waziri Biteko alieleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inaendelea kuboresha miundombinu katika masoko husika ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mashine za kupima madini, mizani na kusomesha wataalam katika fani ya upimaji wa madini.
Katika hatua nyingine, Waziri Biteko alipongeza mgodi wa kuchimba mawe wa Ntyuka uliopo jijini Dodoma kwa kukiwezesha kikundi cha wakinamama 120 kwa kuwapatia
mabaki ya mawe ambayo huyatumia kuzalisha kokoto ambazo huziuza na kujipatia kipato.
Wakati huohuo akizungumza kwa niaba ya kikundi cha wakinamama wanaozalisha kokoto katika eneo la Ntyuka jijini Dodoma Blandina Daudi mbali na kushukuru mgodi
kwa kuwapatia mabaki ya mawe kwa ajili ya kuzalisha kokoto alieleza kuwa kupitia kazi husika wameweza kufanya maendeleo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba na kusomesha watoto.
Awali akizungumza katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati ya Madini katika Soko la Madini la Dodoma, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma,
Laurent Bujashi alisema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa soko husika kwa kipindi cha miezi sita kabla, ukusanyaji wa mapato ulikuwa ni jumla ya shilingi milioni 118.4 ikiwa
ni wastani wa shilingi milioni 23.6 kwa mwezi.
Bujashi aliendelea kueleza kuwa mara baada ya kuanzishwa kwa soko la madini Mei 19, 2019 makusanyo yaliongezeka hadi kufika jumla ya shilingi milioni 486.8 kwa kipindi cha miezi sita ikiwa ni wastani wa shilingi milioni 54.1 kwa mwezi na kusisitiza kuwa ongezeko hilo lilitokana na uwepo wa soko na uwazi katika biashara ya madini hususan dhahabu.