Home Mchanganyiko WWF na Vodacom waadhimisha wiki ya Siku ya Wanawake Duniani Mloganzila

WWF na Vodacom waadhimisha wiki ya Siku ya Wanawake Duniani Mloganzila

0

WWF na Vodacom katika picha ya pamoja mara baada ya kuitembelea Hospitali ya Mloganzila.

Baadhi ya zawadi zilizotolewa hospitalini hapa katika wiki ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Bi. Jackline Ngoni kutoka WWF akimjulia hali na Bi. Khadija Bakari kabla ya kumkabidhi zawadi wakati walipotembelea wodi ya wanawake hospitalini hapa.Baadhi ya wanachama wa WWF na Vodacom wakichangia damu hospitalini hapa.

Baadhi ya washiriki wakipanda miti katika eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila leo.

************************************

Shirika la Kimataifa la Utunzaji Mazingira (WWF-Tanzania) kwa kushirikiana na Vodacom wanawake wameitembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila na kupanda miti, kutoa zawadi kwa wagonjwa katika wodi ya wanawake na
kuchangia damu kwa lengo la kujenga ushirikiano na jamii wakati wa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika tarehe 8 Machi mwaka huu.

 

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi katika wodi ya wanawake iliyopo hospitalini hapa, Meneja Mawasiliano wa Shirika la Kimataifa la Utunzaji Mazingira (WWF-Tanzania), Bi. Joan Itanisa amesema wameamua kuitembelea
hospitali kwa nia ya kujenga ushirikiano na jamii kwa kutoa zawadi na kushiriki katika kutunza mazingira kama sehemu ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani.

 

“Tumeamua kutoa zawadi mbalimbali kama vile blanketi, pampasi za watoto na watu wazima, kofia, mafuta ya nazi, tishu za kujifutia kwa watoto (baby wipes) na soksi tunaamini zitawasaidia wagonjwa waliopo hospitalini hapa” amesema Bi. Itanisa.

 

Meneja Ruzuku na Mawasiliano wa Vodacom Foundation, Bi. Sandra Oswald amesema matembezi haya yanaenda sambamba na mkakati wa Taifa wa utunzaji mazingira na nia hasa ni kusambaza ujumbe kwa jamii inayotuzunguka juu ya umuhimu wa kutunza mazingira.

 

“Katika kuadhimisha wiki ya siku ya wanawake duniani sisi wanawake leo tumeshiriki kutunza mazingira kwa kupanda miti katika Hospitali ya Mloganzila kama sehemu ya kuhifadhi mazingira yanayozunguka hospitali hii” amesema Bi. Oswald.

 

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi MNH-Mloganzila, Sr. Redemptha Matindi amewashukuru WWF-Tanzania pamoja na Vodacom kwa kuitembelea Hospitali ya Mloganzila,
kutoa zawadi na kuchangia damu kwa lengo la kuokoa maisha ya watu mbalimbali wenye uhitaji wa damu.