Home Mchanganyiko NAIBU WAZIRI IKUPA AUNGANA NA WANAWAKE WA MOI KUPELEKA MAHITAJI MAALUM KWA...

NAIBU WAZIRI IKUPA AUNGANA NA WANAWAKE WA MOI KUPELEKA MAHITAJI MAALUM KWA WAGONJWA HOSPITALINI HAPO.

0

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Bunge , Sera ,Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe.Stella Ikupa katikati akimkabidhi mwakilishi wa wazazi ambao watoto watoto wao wana vichwa vikubwa na migongo wazi wa kwanza kulia baadhi ya mahitaji wakati wa kugawa mahitaji mbalimbali kuelekea kilele cha siku ya wanawake Duniani iliyofanyika leo katika Taasisi ya Mifupa MOI , wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Respicious Boniface

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Bunge , Sera ,Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe.Stella Ikupa wa pili kulia akiongea na wazazi ambao watoto watoto wao wana vichwa vikubwa na migongo wazi wakati wa kugawa mahitaji mbalimbali kuelekea kilele cha siku ya wanawake Duniani iliyofanyika leo katika Taasisi ya Mifupa MOI , wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Respicious Boniface.

************************

Na Mwandishi Mwandishi wetu.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera , Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa ameungana na Umoja wa wanawake kutoka Taasisi ya mifupa MOI kutoa mahitaji mbalimbali kwa Watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi leo jijini dar es salaam kuelekea kilele cha siku ya wanawake Duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi mahitaji hayo Mhe. Stella amesema kuwa ni vyema kuwakumbuka wenye mahitaji maalum hasa wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ili kuwapunguzia gharama wazazi wao za kuwatibia na kuwahudumia.

“Kama tunavyofahamu Watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi wana changamoto kubwa hasa katika mifumo ya mwilini hivyo leo tumeleta mahitaji mbalimbali ili kuwapunguzia hadha wazazi wao pindi wanapopata huduma hapa hospitalini”,alisema Mhe. Stella.

Aidha Mhe. Stella amewataka wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi katika shughuli za kijamii hususan kuwapa mahitaji wale ambao wanahuitaji ikiwemo wagonjwa hospitalini ili kuwarahisishia kumudu gharama za matibabu na mahitaji mengine.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Respicious Boniface amesema kuwa mahitaji hayo yatawasaidia Watoto hao katika matumizi mbalimbali na kuwapa faraja wazazi na walezi ili wasikate tamaa katika kuwaangalia Watoto wao.

“Nitoe rai kwa wazazi au walezi wasiwafiche Watoto wenye vichwa vikubwa na matatizo kama hayo na badala yake wawalete hospitali kwa taratibu za kitabibu zaidi na pia wazazi wanatakiwa kula vyakula vyenye rutuba wanapokuwa wajawazito ili kuweza kuzuia matatizo hayo”, alisema Dkt. Respicious.

Aidha Dkt. Respicious amewataka wanawake hao ambao ni wahudumu wa afya pamoja na madaktari kutoka MOI waendelee kusapoti juhudi za Serikali katika kuleta afya bora kwa kuzingatia miiko na maadili ya kazi zao na kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa wote.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake MOI Bi. Elizabeth Mrindoko amesema kuwa wana utaratibu huo wa kutoa mahitaji maalum kwa Watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi takribani mwaka wa pili sasa kwa kutambua changamoto zinazowapata wazazi na walezi wa Watoto hao.

“Nawashukuru Wanawake wa MOI kwa kujitolea kwao lakini ningependa kujitolea huko pia kuendelee katika kuwapa huduma wagonjwa waliopo katika Taasisi yetu ili wapone haraka na kurudi kwenye majukumu yao ya kila siku wakiwa na afya iliyoimarika”, alisema Bi. Mrindoko.

Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambayo hufanyika Aprili 8 kila mwaka Naibu waziri Stella ameungana na Umoja wa wanawake kutoka MOI, TUGHE na FINCA kutoa mahitaji mbalimbali ikiwemo pampasi, Mafuta ya kupaka, sabuni za kuogea na kufulia na vyakula kwa watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi.